Na Mwandishi wetu, Babati
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Regina Ndege amekabidhi mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Magugu Wilayani Babati Mkoani Manyara.
Naibu Waziri Regina ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara, ameshiriki Ibada ya misa takatifu ya kipaimara kwenye Parokia ya Magugu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu, mhashamu Anthony Lagwen.
Naibu Waziri Regina katika ibada hiyo amejitolea kiasi cha mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hilo ambapo pia kulifanyika harambee na kupatikana fedha taslimu kiasi zaidi ya shilingi milioni 12.
Naibu Waziri Regina akizungumza kwenye harambee hiyo ameliomba Kanisa kuliombea Taifa, kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Mhe Regina aliambatana na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Manyara, Fatuma Tsea, Diwani wa Kata ya Magugu, Mhe. Stanley Dismas na Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Stahimili Masasi.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbulu mhashamu Anthony Lagwen amemshukuru Naibu Waziri Regina kwa majitoleo yake ya ujenzi wa Kanisa hilo la Magugu.

