Wadau wa sekta ya nishati nchini wametakiwa kuhakikisha maazimio yaliyotokana na Kongamano la Wiki ya Nishati Jadidifu 2026 yanatekelezwa kwa vitendo ili kuleta matokeo yanayopimika na kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati nchini.

Wito huo umetolewa Novemba 13, 2026 na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Mhandisi Imani Mruma, wakati akifunga Kongamano la Wiki ya Nishati Jadidifu 2026 (Renewable Energy Week 2026), lililoandaliwa na Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.

Amesema ni muhimu wadau kuweka nguvu katika uwekezaji wa nishati jadidifu, matumizi bora ya nishati na kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati nchini.

Amesema Tanzania inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na kujiandaa kufikia megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050, malengo yanayohitaji kuongeza vyanzo vya nishati, kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

 Amesema Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa megawati 150, ambapo awamu ya kwanza ya megawati 50 imeanza kufanya kazi, ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo hayo.

Ameeleza kuwa kongamano hilo limejadili maeneo muhimu ya maendeleo ya sekta ya nishati, yakiwemo mchango wa nishati jadidifu katika kukuza viwanda, nishati safi ya kupikia, matumizi ya nishati katika shughuli za uzalishaji, ufanisi wa nishati, usafiri unaotumia umeme, ushiriki wa wanawake na vijana pamoja na fursa za uwekezaji.

Akizungumzia utekelezaji wa maazimio hayo, Mhandisi Mruma amezitaka taasisi za Serikali, TANESCO, EWURA, REA, TGDC, TBS, sekta binafsi, taasisi za fedha, wawekezaji, washirika wa maendeleo na taasisi za elimu kuimarisha ushirikiano na uratibu ili kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa yanatekelezwa kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa kila taasisi inapaswa kubainisha maeneo ya kipaumbele yanayohusu majukumu yake, kuweka muda wa utekelezaji na kushiriki katika kufuatilia maendeleo ya kazi hizo ili kubaini na kuondoa changamoto za kisera, kiufundi na kifedha zinazokwamisha maendeleo ya sekta.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza programu za nishati safi ya kupikia na usafiri wa umeme, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kuandaa miradi inayokidhi vigezo vya kupata ufadhili na uwekezaji. Pia, ameeleza umuhimu wa kuweka utaratibu wa pamoja wa kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya kongamano hilo.

Vilevile, ameipongeza TAREA kwa kutimiza miaka 25 ya mchango wake katika kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu nchini.

Amesema Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha mapendekezo na fursa zilizobainishwa katika kongamano hilo zinachangia utekelezaji wa sera na mikakati ya Taifa, hususan kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.