Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wilaya ya Mbagala, Bi. Verdiana Ndamgoba (kulia), akizungumza na mtangazaji wa Clouds FM, Geah Habibu (kushoto), kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wakati wa Tamasha la Malikia wa Nguvu lililofanyika leo, Novemba 13, 2026, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Msufini, Chamazi, jijini Dar es Salaam

…….

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Temeke, limehamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutoa elimu kwa wakazi wa Kata ya Chamazi kuhusu matumizi ya majiko ya umeme, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa pamoja na kulinda afya za wananchi na mazingira.

Akizungumza leo Novemba 13, 2026, katika Tamasha la Malikia wa Nguvu lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Msufini, Chamazi, Dar es Salaam, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Wilaya ya Mbagala, Bi. Verdiana Ndamgoba, amesema matumizi ya umeme kupikia yana faida nyingi, ikiwemo kuokoa muda kutokana na uwezo wa majiko ya kisasa kuandaa chakula kwa haraka.

Ndamgoba amesema matumizi ya majiko hayo yanasaidia kupunguza moshi unaotokana na uchomaji wa kuni na mkaa, ambao unaweza kuathiri afya za watu na mazingira, huku akieleza kuwa TANESCO inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na salama ya umeme, namna ya kutumia vifaa vya kupikia kwa ufanisi na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza manufaa ya nishati hiyo katika maisha ya kila siku.

Amewahimiza wananchi kuzingatia kanuni za usalama wanapotumia umeme majumbani na maeneo ya kazi, akisisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha ajali, majeraha na uharibifu wa mali.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Chamazi walioshiriki tamasha hilo wameishukuru TANESCO kwa kuwapatia elimu hiyo, wakieleza kuwa imewaongezea uelewa kuhusu matumizi salama ya umeme, huduma zinazotolewa na shirika pamoja na njia za kuwasiliana na taasisi hiyo wanapohitaji msaada au kutoa taarifa za hitilafu.

Katika tamasha hilo TANESCO wametoa elimu kwa vitendo kwa kupika chakula kupitia majiko ya umeme pamoja na kuwaelimisha huduma za kidijitali zikiwemo LUKU Janja na NIKONEKT JISOTI, ambazo zimekusudiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha mawasiliano kati ya shirika na wateja wake.