Tanzania inatarajia kupokea wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika watakaotembelea nchini kwa lengo la kujifunza kwa vitendo uzoefu na mikakati inayotumika kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, kupitia uwekezaji katika miundombinu, rasilimali watu na mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya afya.
Hatua hiyo inalenga kutumia uzoefu wa Tanzania katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kuwa mfano wa kujifunza kwa mataifa mengine ya Afrika, hususan katika kuimarisha huduma hizo na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya kina mama na watoto wachanga.
Akizungumza Novemba 13, 2026, wakati wa ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Katoro, mkoani Geita, Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema Sekretarieti inatarajia kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika watakaotembelea Tanzania kwa lengo la kujifunza kwa vitendo kuhusu uwekezaji katika sekta ya afya, hususan katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa AU wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, amedhamiria kuendeleza uwekezaji katika afya ya mama na mtoto barani Afrika. Hivi karibuni tutaanza kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kuja kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua katika kuboresha huduma, ili waweze kuchukua uzoefu huo na kwenda kuutumia katika nchi zao,” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Amesema ziara yake katika Hospitali ya Wilaya ya Katoro imelenga kuona maendeleo ya ujenzi wa wodi maalumu ya watoto wachanga sambamba na kujionea namna huduma hizo zinavyotolewa ili kutumia uzoefu huo kuhamasisha na kusaidia nchi nyingine za Afrika kuimarisha huduma hizo. Katika ziara hiyo, Mhe. Ummy amepokea taarifa ya ujenzi wa wodi maalumu ya watoto wachanga ambao umefikia asilimia 60 ya ujenzi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omari Sukari, amesema mkoa huo umepiga hatua katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, ambapo vituo vinavyotoa huduma za upasuaji wa dharura vimeongezeka kutoka 18 mwaka 2021 hadi 35 kwa sasa huku zaidi ya vituo 61 vya kutolea huduma za afya vimeongezeka katika kipindi cha miaka mitano, hatua iliyosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
“Hospitali ya Wilaya ya Katoro ina jengo maalumu lenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watoto 60, huku jengo jingine linalojengwa katika ngazi ya mkoa likitarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watoto 160” amesema Dkt. Sukari.
Ameongeza kuwa hospitali hiyo imeimarisha rasilimali watu kutoka watumishi wasiopungua 30 ilipoanza kutoa huduma hadi kufikia watumishi 72 kwa sasa, wakiwemo wataalamu zaidi ya 40, huku watumishi wengine 20 wakiongezwa ili kuimarisha utoaji wa huduma.
Dkt. Sukari ameishukuru Serikali na Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana katika uwekezaji wa miundombinu maalumu ya kuwahudumia watoto wachanga, akisisitiza kuwa mkoa utaendelea kuhakikisha majengo hayo yanakuwa na watumishi wa kutosha, vifaa tiba na yanatunzwa vizuri ili wananchi wanufaike na huduma bora.

