* Azindua Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema zaidi ya majengo 140 ya halmashauri yamejengwa katika kipindi cha miaka minne hadi mitano, akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo unaoboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Majengo ya aina hii, ndani ya kipindi cha miaka minne na kwenda mitano, yamejengwa zaidi ya 140,” amesema.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 13, 2026), wakati akizindua Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.
Amesema uwekezaji huo umezinufaisha pia halmashauri kongwe zilizokuwa zikitumia majengo yasiyokidhi mahitaji yao, huku watumishi wakikabiliwa na uhaba wa nafasi za ofisi.
Waziri Mkuu amesema Ludewa ni miongoni mwa halmashauri hizo, na kwamba kukamilika kwa jengo hilo ni hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Khalid A. Khalif, amesema jengo hilo limeondoa changamoto ya wananchi kufuata huduma katika ofisi zilizokuwa maeneo tofauti.
Amesema Halmashauri hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1982, haikuwa na jengo mahususi la makao makuu hadi ujenzi wa mradi huo ulipoanza mwaka 2021.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, Serikali imetoa shilingi bilioni 3.67, ambapo shilingi bilioni 3.49 zimetumika kukamilisha ujenzi. Fedha zilizobaki zimepangwa kununua samani katika awamu ya pili.
Jengo hilo lina sakafu ya chini na ghorofa moja juu, pamoja na kumbi mbili za mikutano. Linajumuisha ofisi za Mkurugenzi Mtendaji, idara na vitengo vya Halmashauri.

