Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme, hususan nyakati za jioni, itapatiwa ufumbuzi kupitia kukamilika kwa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Songea–Tunduru–Masasi.

Ameyasema hayo Novemba 12, 2026, wakati wa ziara yake wilayani humo ambapo ameeleza kuwa anatambua changamoto ya kukatika kwa umeme inayosababishwa na kushuka kwa kiwango cha volteji, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto hiyo.

Aidha, amesema Serikali imechukua hatua dhidi ya Mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi wa umeme kutoka Tunduru kutokana na kuchelewesha utekelezaji wake.

 Ameongeza kuwa TANESCO imebadilisha wasimamizi wa mradi huo kwa kuweka timu mpya ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Amesisitiza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika na endelevu.