Na Sixmund Begashe, Arusha
MFUKO wa Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TWPF) umekuwa moja ya nguzo imara ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini kutokana na namna unavyosaidia zaidi taasisi za Uhifadhi kwenye nyanja hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania Prof. Jafari Kideghesho kwenye kikao cha 93 cha Bodi hiyo jijini Arusha.
Prof. Kideghesho amesema kuwa kabla ya kikao hicho, Wajumbe wa Bodi hiyo walipata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na taasisi za Uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia fedha za mfuko huo.
Amesema kuwa kwa ujumla Bodi imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo hatua inayoonesha thamani halisi ya fedha zilizo tolewa na TWPF.
“Hatua hii kubwa na ujenzi wa miradi hii inadhihirisha kuwa, Wizara kupitia taasisi zake inasimamia vyema hivyo sina budi kuipongeza Wizara kwa kazi hii kubwa na nzuri,” alisema Prof. Kideghesho.
Pamoja na kuwataka wanufaika wa Mfuko huko kukamilisha miradi kwa wakati, katika kikao hicho Pro. Kideghesho amesema Bodi imeelekeza wasimamizi wa Mfuko huo kuhakikisha unaendelea kuendana na malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi wa Wanyapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora pamoja na kuishukuru Bodi hiyo kwa mchango wake mkubwa kwenye usimamizi na uendelezaji wa Mfuko huo, amesema ofisi yake itayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolea kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kabla ya kikao hicho, wajumbe wa Bodi hiyo walitembelea Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kukagua ujenzi wa uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori wakali na waharibifu kufika katika maeneo ya wananchi na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) katika Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Utawala na Maabara.

