Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wahitimu wa vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kusubiri kuajiriwa, akisema mazingira ya sasa yana fursa nyingi zinazoweza kutumiwa na vijana.

Alisema mhitimu anayemaliza mafunzo ya ufundi anapaswa kuwa na uwezo wa kutambua changamoto zilizopo katika jamii na kuzigeuza kuwa fursa za kujipatia kipato, badala ya kukaa nyumbani akilalamika kukosekana kwa ajira.

Chalamila ametoa wito huo leo Novemba 12,2026 Dar es Salaam wakati akizungumza katika mahafali ya 56 ya chuo cha VETA Dar es Salaam, ambapo amewataka wazazi kuacha kuwakatisha tamaa watoto wao wanaochagua elimu ya ufundi stadi kwa kuiona kama njia ya watu walioshindwa katika masomo.

Amesema VETA ni taasisi yenye heshima inayowawezesha vijana kukuza ndoto zao, kupata maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kujitegemea kiuchumi, hivyo elimu hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa chaguo la mwisho kwa wanafunzi.

Amesema vijana wanapaswa kuelewa kuwa kuhitimu katika taasisi hiyo ni hatua ya kuongeza thamani ya uwezo walionao, hivyo wanapaswa kuondoka chuoni wakiwa na mtazamo mpya wa maisha na utayari wa kutumia ujuzi wao kujenga uchumi.

“VETA siyo mahali pa kukimbilia walioshindwa, VETA ni mahali pa watu kuja kuwa na ndoto, kuzikuz­a ndoto na kuzifanya ndoto kuwa kweli,” amesema Chalamila.

Amesema Dar es Salaam ina fursa nyingi za kiuchumi kutokana na uwepo wa viwanda zaidi ya 1,000 na shughuli mbalimbali za biashara, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia ujuzi wao kutafuta nafasi katika sekta hizo.

Ametoa mfano wa wahitimu waliosomea mitindo ya mavazi, uchapishaji na ufundi wa magari, akiwataka kutumia taaluma zao kuanzisha huduma na biashara zinazohitajika katika soko badala ya kusubiri nafasi za ajira zitangazwe.

Aidha, amewataka wahitimu kufuatilia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wajasiriamali, pamoja na kutafuta mitandao ya kibiashara na taasisi zinazoweza kuwasaidia kukuza shughuli zao.

Chalamila pia amesisitiza umuhimu wa uaminifu na bidii katika kazi, akisema wahitimu watakaopata ajira wanapaswa kulinda mali za waajiri wao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili kujenga imani na kupata nafasi zaidi za maendeleo.

Amesema vijana wanapaswa kujiwekea malengo ya miaka mitano hadi kumi na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia mafanikio, akiwataka kutokata tamaa kutokana na mazingira ya familia zao au hali zao za kiuchumi walikotoka.

Kwa upande wake mkuu wa chuo cha VETA Dar es Salaam,Abraham Mbughuni, ameeleza kuwa chuo kinakabiliwa na changamoto ya uchache na uchakavu wa vitendea kazi vya kufundishia, hali inayokwamisha utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kila mwaka.

Aidha Mbughuni, amesema wanahitaji mabasi mawili, malori mawili aina ya semi-trailer, magari 20 ya mafunzo ya udereva wa awali, pamoja na mitambo ya forklift na vifaa vingine ili kuboresha mafunzo ambapo amesema kwa sasa chuo kina magari 11 ya mafunzo ya udereva wa awali, yanayokidhi kuwahudumia wanafunzi takribani 400 kwa mwezi, huku mahitaji yakiwa makubwa zaidi.

Amesema changamoto nyingine ni uhaba wa majengo na madarasa ya kufundishia, samani na vifaa vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia. Alisema chuo hicho pia kina wahitimu 20 wenye mahitaji maalumu wanaohitaji mitaji na vifaa vya kuwawezesha kujiajiri, akitolea mfano mhitimu Francis aliyebuni chaja ya kompyuta mpakato na ambaye sasa anatumika pia kama mkufunzi chuoni hapo.