NA DENIS MLOWE, MAFINGA

MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele, ameitaka Halmashauri ya Mji Mafinga kuchunguza mfumo wa ukusanyaji wa ada za leseni za biashara na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watumishi wanaotuhumiwa kutumia vibaya mamlaka yao, kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kutozwa fedha na faini zisizoeleweka.

Lutevele ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo, akieleza kuwa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu usimamizi wa biashara, utoaji wa leseni, namba za malipo na namna wafanyabiashara wanavyotozwa faini.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakielezwa kuwa leseni walizonazo haziruhusu kufanya shughuli fulani, hivyo kulazimika kukata leseni nyingine, huku wengine wakitozwa faini kwa viwango ambavyo havijaelezwa kwa uwazi.

Mbunge huyo ameeleza pia kuwepo kwa madai ya wafanyabiashara kutengenezewa namba za malipo ya faini, hali iliyozua maswali kuhusu uhalali wa makusanyo hayo na iwapo fedha zote zinaingia katika akaunti rasmi za halmashauri.

Akitoa mfano, Lutevele amesema kuna mfanyabiashara mwanamke aliyekuwa akiendesha saluni na kuuza bidhaa za nywele aina ya lasta, lakini alidaiwa kuambiwa leseni ya saluni haimruhusu kuuza bidhaa hizo, akafungiwa biashara na kutozwa faini.

Aidha, ameeleza kutoridhishwa na madai ya baadhi ya wafanyabiashara kufungiwa biashara zao hadi saa nne usiku, akisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri haupaswi kugeuka chanzo cha kero, vitisho au gharama zisizoeleweka kwa wananchi.

Malalamiko hayo yaliungwa mkono na Diwani wa Kata ya Boma, Baraka Kisakanike, ambaye amesema amekuwa akipokea taarifa nyingi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu namna wanavyosimamiwa, ikiwemo kufungiwa biashara na kutozwa faini ambazo hawazielewi utaratibu wake.

Kisakanike amesema wafanyabiashara hawapingi kulipa kodi, ada na tozo zinazostahili, lakini wanahitaji mfumo ulio wazi unaowapa nafasi ya kutekeleza wajibu wao bila kukumbana na usumbufu usio wa lazima.

Kutokana na malalamiko hayo, Baraza la Madiwani limetaka uongozi wa halmashauri kumhamisha kituo cha kazi Afisa Biashara Baraka Mbumba, ambaye ametajwa katika tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma na matumizi yasiyo sahihi ya mamlaka katika usimamizi wa wafanyabiashara.

Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Peter Ngussa, amesema uongozi utayafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na madiwani, yakiwemo yanayohusu watumishi na usimamizi wa shughuli za biashara.

Ngussa amefafanua kuwa suala hilo lilianza kujadiliwa katika kikao cha Kamati ya Fedha kilichofanyika wiki iliyopita, ambapo hatua za awali za kiutawala zilianza kuchukuliwa kwa kumtaka mtumishi huyo asishiriki katika shughuli za nje za kikazi wakati suala hilo likifuatiliwa.

Ameahidi kuwa halmashauri itazingatia maelekezo ya Baraza la Madiwani pamoja na yale ya Mkuu wa Wilaya, huku akisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.