Na Farida Mangube Morogoro

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wanamichezo nchini kutumia nafasi zao kuwa sauti ya jamii katika kupinga vitendo vya mmomonyoko wa maadili na kuwa mfano wa malezi bora, akisisitiza kuwa wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kujenga jamii yenye nidhamu na misingi imara ya kimaadili.

Dkt. Nchemba amesema hayo Novemba 12, 2026, mjini Morogoro wakati akifungua rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMUTA), akieleza kuwa vitendo vinavyodhoofisha maadili havipaswi kufumbiwa macho kwa kuwa vinaathiri ustawi wa nguvu kazi na maendeleo ya Taifa.

Amesema wanamichezo wana wajibu wa kuwa kioo cha jamii kwa kuonesha mwenendo unaozingatia maadili, huku akiwataka kuimarisha nidhamu ndani na nje ya viwanja vya michezo na kutambua kuwa kushinda na kushindwa ni sehemu ya ushindani wa kimichezo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amewahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya michuano ya AFCON, akieleza kuwa tukio hilo kubwa la kimataifa ni fursa muhimu kwa nchi kuimarisha miundombinu, kuitangaza Tanzania na kukuza mshikamano wa kitaifa. Amesisitiza umuhimu wa kujenga hamasa, umoja, uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi ili kuhakikisha Taifa linakuwa sehemu ya mafanikio ya kihistoria ya michuano hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, amesema mashindano hayo yana mchango chanya katika kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa huo kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara zinazochochewa na ujio wa washiriki na wageni wanaohudhuria mashindano hayo.

Naye Mwenyekiti wa SHIMUTA, Marcel Bituro,amesema mashindano ya SHIMUTA mwaka huu yamewakutanisha washiriki 4,500 kutoka taasisi 96, watakaoshindana katika michezo mbalimbali.