Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha leo 

Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha 

…………

Na Happy Lazaro, Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya miundombinu ya barabara na viwanja vya michezo, akisema uwekezaji huo unaimarisha maandalizi ya Mkoa wa Arusha kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2027.

Makalla ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifunga kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, ambapo amesema wilaya zote za mkoa huo zimeendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kupitia fedha za Serikali.

Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya Rais Samia ya kuboresha miundombinu na kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi, huku akieleza kuwa bodi hiyo imeazimia kuendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia bajeti zilizotengwa.

Amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti ni muhimu katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi inatoa matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, Makalla amesema mkoa umejipanga kuhakikisha miradi ya miundombinu inayohusiana na michuano hiyo inakamilika, huku akiwapongeza wananchi kwa ushirikiano wao katika kupisha utekelezaji wa miradi, ikiwemo ujenzi wa barabara zinazoelekea katika uwanja wa michezo.

Ameeleza kuwa Serikali pia inalenga kuunganisha ukumbi mpya wa kimataifa wa mikutano unaojengwa eneo la Kijenge jijini Arusha na mtandao bora wa barabara, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri na kurahisisha shughuli za mikutano na matukio ya kimataifa.

” Mkoa unatarajia kuunganisha ujenzi wa ukumbi mpya wa kimataifa wa mikutano unaojengwa Kijenge na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ikiwemo barabara ya njia nne na ujenzi wa barabara ya juu (Flyover), kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na TAMISEMI,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, akieleza umuhimu wa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya, ameeleza kuridhishwa na kasi ya usimamizi wa miradi inayotekelezwa mkoani humo, huku akimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Baraka Messiaky, pia amempongeza Makalla kwa usimamizi wa miradi hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya viongozi na wadau kuhakikisha miradi inakamilika na kuwanufaisha wananchi.