Na Jackline Minja WMJJWM – MBEYA
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanawake wanaoomba mikopo hawawekewi vikwazo visivyo vya lazima vinavyoweza kuchelewesha upatikanaji wa mikopo hiyo, badala yake wawasaidie kukamilisha taratibu zinazohitajika ili wanufaike na fursa hizo kwa wakati.
Mhe. Mahundi ameyasema hayo Novemba 12, 2026, wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Mbeya, ambapo amesema uwezeshaji wanawake kiuchumi unahusisha kuwapatia fursa, rasilimali, ujuzi, mitaji na teknolojia ili washiriki kikamilifu katika biashara, kilimo, viwanda na shughuli nyingine zinazozalisha kipato.
“Maafisa maendeleo ya Jamii ni kiungo muhimu katika kuwawezesha wanawake kupata mikopo na fursa za kiuchumi, hivyo wanapaswa kuwa karibu nao, kuwapa maelekezo sahihi na kuwasaidia katika hatua mbalimbali za maombi ya mikopo.
” Tusiwe tunafanya haya makongamano kama fasheni, yawe njia nzuri ya kukumbushana kuwahudumia wananchi tuache longolongo” amesema Mhe. Mahundi
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado wanawake wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mikopo, mitaji na mazingira ya kibiashara, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuimarisha mifumo ya kifedha.
Aidha, ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kuonesha kuwa wanawake ni asilimia 52 ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya, sawa na watu 1,219,926, jambo linalodhihirisha umuhimu wa kuwawekea mazingira bora ya kiuchumi.
Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amesema elimu inayotolewa kwa wanawake kuhusu uwezeshaji kiuchumi ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kushiriki katika maendeleo.
Awali, akisoma risala, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoa wa Mbeya, Neema Kisanga, amewasilisha salamu na maoni ya jukwaa kuhusu umuhimu wa kuendeleza juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
Kongamano hilo limewakutanisha viongozi, wadau na wanawake wajasiriamali kwa lengo la kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili wanawake katika shughuli za kiuchumi, pamoja na kuweka mikakati ya kuzitatua.

