Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Novemba 11, 2026
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, ametoa Sh milioni 10 kwa ajili ya kusaidia ofisi za Misikiti ya Kongowe na Ofisi ya Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Pwani iliyopo Mwanalugali, Kibaha.
Koka ametoa fedha hizo wakati akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mariam Abdala, mke wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini, Yahaya Mtonda.
Amesema ameguswa na mahubiri ya Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Abbas Mtupa, yaliyohimiza waumini kutoa sadaka kwa ajili ya kumrehemu marehemu, akieleza kuwa ameamua kuchangia fedha hizo kama sehemu ya kutekeleza mawaidha hayo.
Amesema fedha hizo zitagawanywa kwa ofisi hizo mbili, kila moja ikipata Sh milioni tano kwa ajili ya sadaka ya kumtolea marehemu.
Awali, akitoa mawaidha, Sheikh wa Mkoa wa Pwani, Abbas Mtupa, amewataka waumini kutokata tamaa wanapokumbwa na mitihani ya maisha, bali waendelee kumtegemea Mungu na kuzingatia maelekezo ya dini.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amesema msiba huo ni pigo kubwa, hivyo amewataka viongozi na wananchi kuendelea kushirikiana na familia ya marehemu.
Akitoa salamu kwa niaba ya familia na Wilaya ya Kibaha, Sheikh Said Mtonda, amesema wanashukuru kwa mshikamano na pole walizopokea, akieleza kuwa wanatambua kuwa yote yaliyotokea ni mipango ya Mungu

