Dar es Salaam. Waandishi wa Habari wametakiwa kujithamini kwa kuzingatia mwonekano, mwenendo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuwa namna wanavyojitambulisha inaweza kujenga au kupunguza imani ya vyanzo vya habari na jamii kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 11, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Anthony Kipangula, wakati akihitimisha mafunzo ya siku tatu kwa Waandishi wa Habari, watangazaji, waandaaji wa vipindi, wapiga picha na wahariri kutoka Azam Media.

Wakili Kipangula amesema mwonekano wa Mwandishi wa Habari si suala la mavazi pekee, bali ni sehemu ya utambulisho wa kitaaluma inayoweza kuathiri namna anavyopokelewa, kusikilizwa na kuaminiwa na vyanzo vya habari.

“Unapozungumza na chanzo chako cha habari, mwonekano wako unapaswa kumpa sababu ya kukusikiliza hata kabla hujaanza kuzungumza. Hali hiyo humjengea imani kuwa unauelewa wa jambo unalotaka kulizungumzia,” amesema Wakili Kipangula.

Amesisitiza kuwa Mwandishi wa Habari anapaswa kuvaa kulingana na mazingira na hadhi ya tukio analokwenda kuliripoti, hususan shughuli rasmi zinazohusisha viongozi wakuu wa Serikali na wageni wengine mashuhuri.

“Tunapozungumzia kujithamini kama Waandishi wa Habari, ni pamoja na kuzingatia tunavaa nini na tunakwenda wapi. Unapokwenda kwenye tukio maalumu linalohusisha viongozi wakuu, hakikisha unavaa kulingana na shughuli hiyo. Usivae kama unakwenda kuripoti shughuli za michezo uwanjani,” amesisitiza.

Ameeleza kuwa mwonekano usioendana na mazingira ya tukio unaweza kumfanya Mwandishi wa Habari ashindwe kutambulika kwa urahisi kuwa ni miongoni mwa watu wanaotekeleza majukumu rasmi, hali inayoweza kuathiri upatikanaji wa taarifa na utekelezaji wa kazi yake.

Katika hatua nyingine, Wakili Kipangula amezitaka taasisi za umma na binafsi kuwapa ushirikiano Waandishi wa Habari wanaofika katika taasisi hizo kwa ajili ya kukusanya taarifa, ili kuwawezesha kuandaa habari sahihi na zenye manufaa kwa umma.

Amesema Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari kinatambua haki ya kukusanya na kusambaza habari na taarifa kwa mujibu wa sheria, hivyo ushirikiano kutoka kwa taasisi na vyanzo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi, zilizothibitishwa na zenye maslahi mapana kwa Taifa.

“Waandishi wanapofika kukusanya taarifa kwa ajili ya kuzichakata na kuzisambaza kwa maslahi ya umma, ni vyema kuwapa ushirikiano ili waweze kuandaa na kuchapisha habari sahihi kwa manufaa ya nchi,” amesema.

Aidha, amewataka Waandishi wa Habari kujenga utamaduni wa kuisoma na kuielewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria mbalimbali zinazohusu sekta ya habari, ili wafahamu haki, wajibu na mipaka yao wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliandaliwa na JAB kwa lengo la kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, kanuni, maadili, miiko na misingi ya taaluma, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini kwa kujenga uwezo na kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na maadili miongoni mwa Waandishi wa Habari.