Washiriki wa mafunzo ya siku tatu kutoka Azam Media wamesema mafunzo yaliyotolewa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) yamewapa nafasi ya kujitathmini na kutambua maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo leo, tarehe 11 Novemba, 2026, washiriki hao wamesema mada kuhusu sheria, maadili, uthibitishaji wa taarifa, mwonekano na mwenendo wa Mwandishi wa Habari zimewakumbusha kuwa weledi hauishii katika uwezo wa kutafuta na kuripoti habari pekee.
Wamesema mwonekano unaoendana na mazingira ya kazi, matumizi ya lugha yenye staha, kuheshimu vyanzo vya habari na kuthibitisha taarifa ni miongoni mwa mambo yanayojenga uaminifu wa Mwandishi wa Habari mbele ya jamii.
Mshiriki wa mafunzo kutoka Azam Media, Mohamed Wamlume, amesema, “kujifunza ni mchakato endelevu unaomsaidia Mwandishi wa Habari kuimarisha weledi na kutekeleza majukumu yake kwa usahihi na usalama zaidi” .
Amesema mafunzo hayo yamempa fursa muhimu ya kuongeza maarifa yanayolenga kujenga safari bora ya kitaaluma inayozingatia usalama, usahihi wa taarifa na weledi katika Uandishi wa Habari.
Washiriki hao wameiomba JAB kuendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa Waandishi wa Habari na watendaji wengine wa vyombo vya habari, hususan kutokana na mabadiliko ya teknolojia na changamoto zinazoambatana na kasi ya usambazaji wa taarifa kupitia majukwaa ya kidijitali.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha Waandishi wa Habari, watangazaji, waandaaji wa vipindi, wapiga picha na wahariri kutoka Azam Media, kwa lengo la kuimarisha uelewa wao kuhusu sheria, kanuni, maadili na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.




