Na Silivia Amandius ,Bukoba.
Jumla ya kaya 79, zikiwemo kaya za wamiliki wa nyumba 17 na wapangaji 62, zimeathirika na janga la moto lililotokea katika Mwalo wa Igabiro, Kijiji cha Mushozi, Kata ya Kaagya, usiku wa kuamkia Novemba 7, 2026, huku watu wawili wakipoteza maisha.
Akitoa taarifa hiyo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa robo ya kwanza, uliofanyika Novemba 10, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kenneth Haule, alisema moto huo ulianza baada ya mafuta yaliyokuwa yakichemka kusababisha mlipuko wa jiko la gesi, hali iliyochangia moto kusambaa kwa kasi kupitia nguzo na nyaya za umeme.
Alisema watu wawili waliofariki ni mwanaume mwenye umri wa miaka 20 na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne, huku mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita akijeruhiwa na kuendelea kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Kishanje.
Akitoa pole kwa waathirika, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, alitoa wito wa eneo hilo kupangwa vizuri ili kuzuia kujitokeza kwa majanga kama hayo siku zijazo, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwaombea marehemu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Sadoth Ijunga, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya tathmini ya kina ya madhara yaliyotokana na moto huo ili kuiwezesha Serikali kutoa msaada kwa waathirika kadiri ya uwezo wake.
Madiwani walitoa pole kwa waathirika na kupongeza hatua za awali zilizochukuliwa na viongozi kufanya tathmini ya janga hilo. Pia waliitaka Serikali ya Kijiji kuhakikisha wananchi waliopoteza makazi wanapatiwa makazi ya muda na chakula wakati jitihada za kuwasaidia zikiendelea.

