Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
MAADHIMISHO ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 18 mwaka huu kwa kuonesha bunifu mbalimbali za watafiti wa ndani zinazolenga kutatua changamoto za wananchi katika sekta za afya, uvuvi na nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11,2026 jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya kilele hicho, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kuonesha matokeo ya tafiti na ubunifu unaofanywa na Watanzania katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Amesema miongoni mwa bunifu zilizovutia katika maonesho hayo ni Mkanda wa Salama unaolenga kumsaidia mama anayepata tatizo la kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua, chanjo ya samaki pamoja na teknolojia ya kuzalisha gesi ya hydrogen na oxygen kwa kutumia maji.
Kuhusu Mkanda wa Salama, amesema ubunifu huo tayari umefikia hatua ya uzalishaji kupitia kiwanda kilichofunguliwa Kimara Suka jijini Dar es Salaam, huku nchi za nje zikiwemo Rwanda zikionesha nia ya kununua bidhaa hiyo.
Amesema ubunifu mwingine uliooneshwa ni chanjo ya samaki inayolenga kudhibiti magonjwa yanayosababisha vifo vya samaki, hususan vifaranga wanaofugwa kwenye mabwawa, huku teknolojia hiyo ikianza kutambuliwa hata nje ya nchi.
Aidha, amesema Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kimeibua teknolojia ya kutenganisha maji na kupata gesi ya hydrogen na oxygen, ambazo kwa mujibu wa mbunifu zinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kupikia na kusaidia huduma za hospitali.
Hata hivyo, amesema Serikali imeagiza kufanyika kwa tathmini ya usalama na uwezekano wa kiuchumi wa teknolojia hiyo ili kubaini kama inaweza kutumika kwa gharama nafuu na kuwa miongoni mwa matokeo ya tafiti zinazoweza kunufaisha wananchi.
Prof. Mkenda amesema maadhimisho hayo yaliyozinduliwa Julai 2 mwaka huu yamehusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo kliniki ya ubunifu, maonesho ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika viunga vya Bunge pamoja na tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya COSTECH katika kipindi cha miaka 40.
Amesema katika kuadhimisha miaka hiyo, COSTECH pia iliandaa mkutano wa pamoja na wanasayansi na wadau wa tiba jijini Arusha, Novemba 9 mwaka huu, kwa lengo la kuonesha umuhimu wa tafiti katika kuboresha huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa mkutano huo ulijadili namna ya kuimarisha tafiti za tiba asilia ili kubaini ufanisi wa mimea inayotumika kutibu magonjwa, viwango sahihi vya matumizi yake na madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesema tathmini hiyo inahusisha pia tafiti za awali zinazofahamika kama Preclinical Trial, zinazofanyika kwa kutumia wanyama kabla ya dawa kufanyiwa majaribio kwa binadamu, ili kuhakikisha matumizi ya dawa hizo yanazingatia ushahidi wa kisayansi.
Akizungumzia matarajio ya maadhimisho hayo, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya tafiti na ubunifu kupitia taasisi za elimu ya juu, ujenzi wa shule za sayansi kwa wasichana katika kila mkoa, ufadhili wa masomo na Samia Innovation Fund inayosaidia wabunifu kuendeleza mawazo yao hadi hatua ya uzalishaji.
Amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Novemba 18 katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, huku maonesho ya sayansi, teknolojia na ubunifu yakianza Novemba 17.
Ametoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali kujitokeza katika maonesho hayo ili kujionea bunifu zilizozalishwa na watafiti wa ndani, akieleza kuwa ni sehemu ya kuonesha mchango wa COSTECH katika kuendeleza sayansi na teknolojia nchini katika kipindi cha miaka 40.
