
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) kuhakikisha dunia inahama kutoka kwenye ahadi na kwenda kwenye utekelezaji wa vitendo unaoleta matokeo yanayopimika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akihutubia mkutano huo unaofanyika Antalya, Uturuki, Novemba 11, 2026, Rais Samia amesema COP31 inapaswa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha makubaliano yaliyowekwa yanatekelezwa kwa vitendo.
Amesisitiza kuwa utekelezaji huo unahitaji ushirikiano madhubuti wa kimataifa unaojumuisha upatikanaji wa fedha, uhamishaji wa teknolojia na ujenzi wa uwezo ili kuwezesha nchi kutekeleza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia amesema Tanzania inaendelea kujizatiti kutimiza malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, huku akieleza umuhimu wa kuzingatia ajenda ya COP31 ya kuharakisha utekelezaji wa Makubaliano ya Paris.
Ameeleza kuwa tofauti za mazingira na uwezo wa kiuchumi kati ya nchi zinapaswa kutambuliwa katika utekelezaji wa hatua za tabianchi, kwa kuzingatia misingi ya usawa, haki ya tabianchi na majukumu ya pamoja yanayotofautiana kulingana na uwezo wa kila nchi.
Amesema mafanikio ya mkutano huo yanapaswa kupimwa kwa hatua zinazotekelezwa na matokeo yanayopatikana badala ya kutegemea ahadi na malengo yaliyotangazwa pekee.
