Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Baraza la Mawaziri anayesimamia Hazina ya Taifa nchini Kenya Mhe. FCPA John Mbadi, jijini Nairobi, Nchini Kenya. 

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili namna bora ya kutumia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika utekelezaji wa miradi ya barabara, hususan katika maeneo ya uwekezaji, upatikanaji wa fedha na ushirikiano wa sekta hizo katika kuendeleza miundombinu.

Mazungumzo hayo pia yalihusisha kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu mbinu bora za kuandaa, kufadhili na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo, pamoja na mifumo ya ulipaji wa huduma za baadhi ya miundombinu kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inaendelezwa kwa ufanisi na uendelevu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Uwekezaji wa Umma na Usimamizi wa Rasilimali za Serikali, Bw. Cyrell Wagunda, pamoja na viongozi wa Idara ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) nchini Kenya, wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Kefa Seda.

Mhe. Kadogosa na ujumbe wake wapo nchini Kenya kushiriki Mkutano wa 16 wa Afrika kuhusu Ufadhili, Uwekezaji na Ubia katika Miundombinu (Africa PPP 2026), unaofanyika jijini Nairobi na kukutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo, wawekezaji na taasisi za kifedha kujadili fursa na mikakati ya kuongeza uwekezaji katika miradi ya miundombinu barani Afrika.