Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagiza kubadilishwa kwa meneja wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Songea–Tunduru–Masasi–Mahumbika, kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi katika Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, Makamu wa Rais amesema Serikali imetimiza wajibu wake, ikiwemo kumlipa mkandarasi zaidi ya shilingi bilioni 42 katika kipindi kifupi, lakini kasi ya utekelezaji bado hairidhishi.
Ameelekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha mkandarasi anabadilisha Meneja wa Mradi na kuleta timu yenye uwezo wa kusimamia kazi kwa ufanisi ili mradi ukamilike kwa wakati.
Aidha, ameiagiza TANESCO kuongeza usimamizi na kupeleka wataalamu kusaidia kukamilisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Tunduru, badala ya kumwachia mkandarasi jukumu hilo peke yake.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Wilaya ya Tunduru na kuwezesha mikoa ya Lindi na Mtwara kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema hatua hiyo itaongeza fursa za uwekezaji, uanzishwaji wa viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, sambamba na kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha umeme unatumika kuchochea maendeleo ya kiuchumi badala ya kuwasha taa pekee.
