Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Namtumbo, wakati akiwa ziarani mkoani Ruvuma leo tarehe 11 Novemba 2026.

………… 

Namtumbo, Ruvuma. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiagiza Wizara ya Kilimo kutoa maelezo ya haraka kuhusu sababu za kutotekelezwa kwa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kurejesha kwa wananchi nusu ya shamba lenye ukubwa wa takribani ekari 6,500 linalosimamiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.

Agizo hilo linakuja baada ya Makamu wa Rais kubaini kuwapo kwa mkanganyiko wa taarifa kati ya viongozi wa ASA, Wizara ya Kilimo na madiwani kuhusu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Februari 2024, akionyesha kutoridhishwa na hali hiyo huku akihoji iwapo kuna watendaji wanaokwamisha kwa makusudi utekelezaji wa maagizo ya mkuu huyo wa nchi. Akizungumza na wananchi wa Namtumbo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma, Makamu wa Rais amesema maelekezo ya Rais yalikuwa wazi kwamba nusu ya shamba hilo ibaki chini ya ASA kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu, huku nusu nyingine ikirejeshwa kwa wananchi kwa shughuli za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kipato.

“Hapa tunazungumzia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nataka nipate taarifa kwa nini maelekezo ya Rais mpaka leo hayajatekelezwa. Kama kuna watu wa ASA wanaoleta ugumu au wameshikilia maeneo hayo kibabe, tutachukua hatua,” amesema.

Katika mahojiano yaliyotokea mbele ya wananchi, Waziri wa Kilimo na viongozi wa ASA walieleza kuwa sehemu ya ardhi hiyo imetengwa kwa ajili ya wananchi, ikiwemo ekari 1,300 zilizotolewa kwa kitongoji kilichokuwa na makazi, pamoja na eneo jingine la takribani ekari 1,600 lililotengwa kwa matumizi ya wananchi.

Hata hivyo, maelezo hayo yalipingwa na madiwani wa maeneo husika, ambao walidai kuwa wananchi wengi waliokuwa wakitumia ardhi hiyo kabla ya kukabidhiwa ASA bado hawajapatiwa maeneo yao, licha ya maelekezo ya Rais. Diwani wa Kata ya Rwinga alieleza kuwa baadhi ya wananchi walioondolewa katika maeneo hayo hawajapatiwa hata nusu ekari, kauli iliyomfanya Makamu wa Rais kuendelea kuwahoji viongozi wa ASA kuhusu eneo lililobaki na watu wanaolitumia kwa sasa.

Kutokana na mkanganyiko huo, Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Kilimo, kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa na Wilaya, kuhakikisha anapatiwa taarifa kabla ya mwisho wa siku kuhusu sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa agizo hilo, pamoja na kubainisha mahali zilipo takribani ekari 2,100 ambazo matumizi yake yameibua maswali.

“Februari 2024 tulipita hapa, imepita Februari 2025 na Februari 2026. Sasa nataka kujua kwa nini maelekezo haya hayajatekelezwa. Hizi ekari nyingine anazo nani?” amehoji Makamu wa Rais.

Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watendaji watakaobainika kukwamisha utekelezaji wa maelekezo hayo, akieleza kuwa lengo la Rais Samia lilikuwa kuhakikisha wananchi wanapata ardhi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.