Na Silivia Amandius
Bukoba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mh. Sadoth Ijunga amewataka wajumbe wa Baraza la Madiwani pamoja na wakuu wa idara kuhakikisha changamoto zilizobainika katika robo ya kwanza ya mwaka zinapatiwa majibu na kuwekwa mikakati madhubuti ya kuzitatua katika robo inayofuata, ili kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa chema Nov 10, mwaka huu Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa si vyema changamoto zilezile kuendelea kujadiliwa katika vikao mbalimbali bila kuwepo hatua za kuzitatua. Amewataka wataalamu wa kila idara kuandaa majibu na mikakati itakayowezesha changamoto hizo kufanyiwa kazi kwa wakati.
Aidha, amehimiza ushirikiano wa watumishi na viongozi katika kuboresha ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa shughuli za maendeleo, huku akiishukuru timu ya Halmashauri kwa mchango na ushirikiano wao katika kufanikisha ajenda za kikao hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, ametoa wito kwa viongozi na wataalamu wa Halmashauri kuimarisha ushirikiano katika kusimamia miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, akisisitiza kuwa kila kiongozi anapaswa kutimiza wajibu wake katika eneo lake.
Aidha Sima amewataka wataalamu wa elimu kuanza kubaini shule chakavu na kuandaa mipango ya ukarabati kabla ya Januari 2027, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na madarasa mbalimbali.
Ameongeza kuwa Halmashauri itaendelea kufuatilia kero zilizobainika katika kata zote 29, huku akiwataka madiwani na viongozi wa vijiji kuwasilisha changamoto zinazohitaji hatua za haraka. Pia amesisitiza umuhimu wa wataalamu wanaohusika na ajenda za vikao kuhudhuria ili kutoa ufafanuzi na majibu ya uhakika kwa hoja zinazowasilishwa.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kenneth Haule, ametoa taarifa kuhusu ajali ya gari iliyowahusisha wajumbe saba wa Baraza la Madiwani Oktoba 9, 2026, wakati wa ziara ya Kamati ya Fedha.
Haule amesema ajali hiyo ilitokea wakati wajumbe hao wakiwa katika shughuli za kikazi, ambapo gari walilokuwa wakisafiria lilipata uharibifu mkubwa na baadhi ya wajumbe kupata madhara.
Amesema taarifa hiyo imetolewa rasmi ili kuwajulisha wajumbe wa Baraza kuhusu tukio hilo na madhara yaliyotokana na ajali hiyo.

