Afisa Mahusiano wa benki hiyo , Winnifrida Mwacha akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha
Arusha .Benki ya Azania imesema itaendelea kuwaunga mkono wakulima nchini kwa kutoa mikopo ya riba nafuu pamoja na huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga kukuza shughuli za kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.
Benki hiyo imesema kupitia ushiriki wake katika maonyesho ya HortiLogistics Africa 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha, imepata fursa ya kukutana na wakulima, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Akizungumza kuhusu ushiriki huo,Afisa Mahusiano wa benki hiyo , Winnifrida Mwacha amesema maonyesho hayo yameiwezesha benki kutangaza bidhaa na huduma zake zinazolenga wakulima wa mazao mbalimbali, hususan wakulima wa kilimo cha bustani (horticulture).
Amesema benki hiyo inatoa mikopo ya riba nafuu kwa wakulima wa mazao ya bustani pamoja na mazao mengine yakiwemo korosho, mahindi na maharage, ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kupanua shughuli zao za kilimo.
Mwacha amesema benki ya Azania inatoa huduma za mikopo ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kilimo (Asset Financing), ikiwemo matrekta, pampu za umwagiliaji na vifaa vingine vinavyohitajika katika shughuli za uzalishaji.
“Kupitia maonyesho hayo benki imefanikiwa kupata wateja wapya, kufungua akaunti nyingi za wakulima na kutoa fursa za mikopo kwa wale wanaohitaji mitaji ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.”amesema Mwacha.
Ameongeza kuwa mbali na huduma za kifedha, benki hiyo imetoa elimu ya fedha kwa wakulima ili kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za kibenki, usimamizi wa fedha na namna ya kutumia mikopo kukuza biashara zao.
Katika hatua nyingine, amesema maonyesho hayo yamekuwa fursa ya kujenga mahusiano ya kibiashara na makampuni pamoja na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hali inayotarajiwa kuisaidia benki hiyo kupanua wigo wa huduma zake katika sekta ya kilimo.
Ameongeza kuwa , Benki hiyo inawakaribisha wakulima kufungua akaunti za kilimo ambazo zinafunguliwa bila malipo na mteja hupata kadi ya Visa papo hapo, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.
Ametoa wito kwa wakulima kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo akisisitiza kuwa benki ya Azania imejipanga kukidhi mahitaji yao kwa kuwapatia mikopo na huduma mbalimbali zitakazochangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
