Na WMJJWM, Tarime
Wazee wa mila katika Wilaya ya Tarime wametakiwa kuwa mabalozi wa kuwaelimisha watoto, wazazi na jamii kwa ujumla kuhusu madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike, kupitia majukwaa mbalimbali wilayani humo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju ametoa maelekezo hayo Novemba 10, 2026 akiwa katika kijiji cha Ng’erenge’re, kata ya Regisheni, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, akizindua Kampeni ya kutokomeza ukeketaji kwenye Wilaya hiyo.
Mpanju amesema, pamoja na viongozi wa mila, viongozi wa dini, siasa, wazazi nanda walezi wana wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukeketaji.
“Tumekuja kuzindua kampeni hii inayotukumbusha ulinzi na usalama wa mtoto wa kike, hivyo vyote vinakutegemea wewe kiongozi, mzazi na mlezi kwasababu madhara yake tumeyasikia, kampeni hii pia inatukumbusha kuwalinda watoto wote na vitendo vinavyoweza kuharibu ndoto zao” amesisitiza Mpanju.
Amewasisitiza kuwapa fursa watoto ya kupata elimu na kwamba Serikali imewekeza katika elimu bure ili kuwawezesha watoto wanakosa vikwazo.
Aidha, Mpanju amesema Serikali imeanzisha kukamati za ulinzi wa mtoto kwenye shule za msingi na sekondari kupitia Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Awali katika mdahalo ulioendeshwa na Mhamasishaji wa kitaifa, Seleman Bishagazi wananchi wa kata hiyo pamoja na Kata ya Regisheni wameonesha kuelewa elimu inayotolewa na baadhi yao wamekiri kuwa vitendo hivyo ni hatari kwa watoto wa kike kwani vina madhara makubwa ikiwemo kutokwa damu nyingi na hata kupelekea kifo, maumivu makali, kuambukizana magonjwa na migogoro ya ndoa.
Kampeni hiyo ya kutokomeza ukeketaji katika mkoa wa Mara, inaendelea kutolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Taasisi ya Sauti ya Jamii Kipunguni ambaye ni muongozaji wa midahalo ya kijamii pamoja na Taasisi ya Catholic Sisters Network Against Gender Based Violence.

