Meneja wa Programu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kefar Mbongela akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha

…………
Na Happy Lazaro, Arusha
WANATAALUMA kutoka kada mbalimbali nchini wametakiwa kuimarisha ushirikiano na kuongeza ujuzi ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Programu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kefar Mbongela wakati akizungumza kuhusu kongamano la mwaka 2026 la Professional Diversity linalofanyika jijini Arusha na kuwakutanisha wataalamu zaidi ya 500 kutoka kada mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa.
Mbongela amesema kongamano hilo lililoanza Novemba 9 linatarajiwa kuhitimishwa Novemba 13, 2026, limejikita katika kutathmini namna taaluma mbalimbali zilivyojiandaa kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema mjadala huo unahusisha wataalamu wa kada tofauti zikiwemo sheria, ukandarasi, ugavi na ununuzi, afya, ufugaji na rasilimali watu, akieleza kuwa hakuna taaluma inayoweza kufanya kazi kwa kujitenga na nyingine kwa kuwa zinategemeana katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Ameongeza kuwa wanasheria nao wanapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wengine ili kupanua uelewa wao na kuboresha huduma wanazozitoa, huku kongamano hilo likijadili pia matumizi ya Akili Unde (AI), mabadiliko ya tabianchi na ushindani wa wataalamu wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Mbongela amesema ni muhimu vijana wanaojiandaa kuingia katika taaluma mbalimbali kupata ujuzi unaoendana na mabadiliko ya sasa ili waweze kushindana katika soko la ajira na kutumia taaluma zao kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesema kongamano hilo litahitimishwa kwa kushirikisha Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, ambaye anatarajiwa kuzungumzia nafasi ya wataalamu katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Katika hatua nyingine, washiriki wa kongamano hilo wamepatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi, ikiwa ni pamoja na namna sahihi ya kuzikusanya, kuzihifadhi na kuzichakata kwa kuzingatia sheria.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa mawakili, maafisa wa serikali na wanataaluma wengine kuhusu wajibu wao katika kulinda taarifa wanazozipata wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi wa Bodi ya Chama cha Wanataaluma wa Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania.(TPPA) ambaye ni miongoni mwa wakufunzi ,Rachel Magege amesema ulinzi wa taarifa binafsi ni muhimu kutokana na athari zinazoweza kujitokeza pale taarifa hizo zinapotumiwa isivyo sahihi.
Magege amesema changamoto zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuibiwa kwa taarifa binafsi, kutumika nje ya madhumuni yaliyokusudiwa, kuchakatwa vibaya au kupotea, hali inayoweza kuathiri haki na usalama wa wahusika.
Amesema mawakili ni miongoni mwa makundi muhimu yanayopaswa kuwa na uelewa huo kwa sababu katika utekelezaji wa majukumu yao hushughulikia taarifa nyingi za wananchi na taasisi mbalimbali, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanazilinda ipasavyo.
Amefafanua kuwa ,Tanzania ina Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyopitishwa mwaka 2022 na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi iliyoanzishwa mwaka 2024, ambayo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi na taasisi kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo.
Hata hivyo, amesema uelewa mdogo kuhusu sheria hiyo bado ni changamoto nchini, hususan katika ukusanyaji, utunzaji na uchakataji wa taarifa binafsi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wanataaluma na taasisi mbalimbali ili kuimarisha ulinzi wa taarifa hizo.
