Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
10/11/2026 Dodoma inatajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kunufaika na mpango wa uwekezaji wa dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya kimataifa, kufuatia mazungumzo ya awali kati ya Kampuni ya SF Group of Companies Ltd na wawekezaji kutoka Marekani.
Mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuchangia maendeleo ya utalii tiba nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa ziara ya wataalamu na wawekezaji kutoka Marekani na Uingereza katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) hivi karibuni, Mkurugenzi wa SF Group of Companies Ltd, Koka Sylvester ambaye pia ni Mbunge wa Kibaha alisema kuwa mazungumzo na wadau mbalimbali yanaendelea kuhusu fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya afya.
Alieleza kuwa mpango huo unahusisha wadau wa kimataifa katika sekta za afya, teknolojia na uwekezaji kwa lengo la kuchangia juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za afya nchini.
“Mradi huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya afya na kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha utalii tiba ambapo wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi wataweza kupata huduma za matibabu bila kulazimika kusafiri kwenda nchi nyingine,” alisema Koka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo alieleza umuhimu wa ushirikiano na wataalamu wa kimataifa katika kuimarisha huduma za matibabu ya saratani na kubadilishana uzoefu.
Dkt. Msemo alisema wageni hao wamefurahishwa na maendeleo ya huduma zinazotolewa na ORCI na kueleza utayari wao wa kushirikiana na Taasisi hiyo katika kuimarisha huduma za matibabu ya saratani nchini.
Aliongeza kuwa ushirikiano na wawekezaji pamoja na wataalamu wa kimataifa ni fursa muhimu ya kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wa Taasisi katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Naye Michael Levas kutoka Kampuni ya Savei Capital Management LLC ya Marekani, alieleza kufurahishwa na ziara hiyo pamoja na fursa za ushirikiano zilizopo katika kuendeleza sekta ya afya nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya hatua za awali za kutathmini fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha huduma za afya nchini.

