Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma.

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umeanza maandalizi ya uandaaji wa mpango kabambe wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (District WASH Master Plan) katika wilaya 70 kati ya wilaya 128 zinazohudumiwa na wakala huo, kwa lengo la kuweka mfumo madhubuti wa kupanga, kuratibu na kuelekeza uwekezaji katika sekta hizo.

Akizungumza Novemba 10, 2026, jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Amos Mtweve, amesema kuwa mpango huo utasaidia kuondoa changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji bila kushirikisha sekta nyingine zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi, zikiwemo afya na elimu.

Amesema kuwa kupitia mpango huo, RUWASA itashirikiana na wizara, halmashauri na wadau wengine kupanga kwa pamoja miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazohitajika kwa utaratibu unaozingatia mahitaji ya maeneo husika.

Aidha, amebainisha kuwa awali miradi mingi ya maji ilikuwa ikitekelezwa kutokana na maombi kutoka kwenye halmashauri na wabunge, hali iliyokuwa ikileta changamoto ya kuweka vipaumbele na kupanga maeneo ya kuanza na kumalizia miradi, hivyo mpango mpya utasaidia kuweka utaratibu wa utekelezaji kwa awamu.

Pia ameongeza kuwa mpango huo utasaidia kuzuia mwingiliano wa miradi kati ya sekta mbalimbali, ikiwemo changamoto zinazoweza kujitokeza pale RUWASA inapotekeleza mradi wa maji katika eneo ambalo sekta nyingine ina mipango tofauti ya maendeleo.

Kwa upande wake, Afisa Mipango wa RUWASA na Mwenyekiti wa Wash Taifa, Singolile Mwamaja, amesema kuwa utekelezaji wa District WASH Master Plan utazingatia ukusanyaji wa takwimu, tathmini ya mahitaji na uwekaji wa vipaumbele ili kuhakikisha miradi ya maji na usafi wa mazingira inapangwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Amesema kuwa hadi sasa mpango huo umeanza kutekelezwa katika wilaya sita, huku wilaya ya Simanjiro ikiwa katika hatua za utekelezaji, ambapo kazi hiyo inatarajiwa kufanyika kwa siku 103 kuanzia Desemba Mosi hadi Machi 30.

Naye, Meneja wa Programu wa Water for People, Mhandisi Victor Pallangyo, amesema kuwa gharama za uandaaji wa District WASH Master Plan zinategemea ukubwa wa kazi, akitolea mfano wa Wilaya ya Mpwapwa ambako uandaaji wa mpango huo uligharimu takribani shilingi milioni 110, huku asilimia 45 hadi 50 ya gharama hizo zikitumika katika ukusanyaji wa takwimu za awali.

Aidha, amebainisha kuwa mpango huo utasaidia wadau kujua maeneo yanayohitaji uwekezaji na aina ya huduma zinazohitajika, zikiwemo maji, vyoo na usafi binafsi, pamoja na kuratibu shughuli za wadau ili kuzuia kurundikana kwa rasilimali katika eneo moja wakati maeneo mengine yakikosa huduma.

Kwa upande wake, Mratibu wa Afua za Afya na Mazingira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Martha Mariki, amesema kuwa mpango huo ni muhimu katika kuboresha huduma za afya na usafi wa mazingira katika kaya, taasisi na jamii kwa ujumla, hatua itakayosaidia kupunguza magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa huduma hizo.

Kikao kazi hicho cha wadau kuhusu District WASH Master Plan Concept Note na RUWASA District WASH Master Plan Guide kimefanyika kwa lengo la kujadili mwongozo wa uandaaji wa mipango hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku wadau wakihimizwa kutoa ushirikiano wa kitaalamu, takwimu na rasilimali ili kufanikisha utekelezaji wake.