Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Alphonce Mokoki, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .

Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imewekeza Shilingi bilioni 42 katika kuwawezesha wakulima na wadau wa sekta ya mboga mboga na matunda, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Alphonce Mokoki, amesema kati ya uwekezaji wa Shilingi bilioni 42 uliotajwa na benki hiyo, Shilingi bilioni 28.8 zimetolewa moja kwa moja kwa wakulima, huku Shilingi bilioni 13.3 zikitumika kudhamini mikopo ya wakulima wadogo wanaopata mikopo kupitia benki za biashara.

Amesema utaratibu huo unalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo ambao wanaweza kukosa dhamana za kutosha wanapohitaji mikopo katika taasisi za kifedha.

Mokoki ameeleza kuwa kupitia udhamini huo, TADB inapanua wigo wa wakulima kunufaika na huduma za kifedha na kuongeza uwezo wao wa kuwekeza katika shughuli za kilimo.

Mokoki amesema utaratibu huo unalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo ambao wanaweza kukosa dhamana za kutosha wanapohitaji mikopo katika taasisi za kifedha.

Mokoki ameeleza kuwa kupitia udhamini huo, TADB inapanua wigo wa wakulima kunufaika na huduma za kifedha na kuongeza uwezo wao wa kuwekeza katika shughuli za kilimo.

“Uwekezaji huo umewezesha kuwafikia wakulima wengi, wakiwemo wanaume, wanawake na vijana, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika sekta ya kilimo cha mboga mboga na matunda.”amesema Mokoki.

Mokoki amesema TADB imeshiriki maonesho ya HortiLogistica yanayoendelea jijini Arusha kwa lengo la kukutana na wadau mbalimbali, kutangaza huduma zake na kutafuta wateja wapya watakaoshirikiana na benki hiyo kukuza sekta ya kilimo cha bustani.

Amesema uzalishaji wa mboga mboga na matunda nchini unatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 7.5 hadi tani milioni 15, hali inayohitaji uwekezaji zaidi katika uzalishaji, teknolojia, uchakataji na upatikanaji wa masoko.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi, yakiwemo jua kali na mvua zisizotabirika, ni changamoto zinazohitaji wakulima kuimarisha mifumo ya umwagiliaji ili kuendelea kuzalisha bila kutegemea mvua pekee.

Amesema TADB imejipanga kuwawezesha wakulima kutumia mifumo ya umwagiliaji na teknolojia zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi (Climate Smart Agriculture), ili kuongeza ustahimilivu na kuimarisha uzalishaji wa mazao.

Aidha, amesema benki hiyo inahimiza wakulima kupata vyeti vya ubora wa mazao (certifications) kwa kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na wadau pamoja na mamlaka zinazohusika na utoaji wa vyeti hivyo.

Amesema utaratibu huo unasaidia kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa mazao (traceability), kuanzia hatua za uzalishaji hadi yanapofikishwa sokoni, na kuhakikisha yanakidhi viwango vinavyohitajika katika masoko mbalimbali.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa vyeti hivyo ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyozingatiwa na benki hiyo wakati wa kutoa mikopo, ili kuhakikisha wakulima wanaowezeshwa wanafuata viwango vinavyotambulika.

Mokoki amesisitiza kuwa TADB iko tayari kushirikiana na wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji katika kuongeza mitaji, kupanua masoko na kuwezesha mazao ya Tanzania kufikia masoko ya kimataifa.

Amehitimisha kwa kuwataka wadau wa sekta ya mboga mboga na matunda kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo, akieleza kuwa uwekezaji katika mitaji, teknolojia na ubora wa mazao ni muhimu katika kukuza sekta hiyo na kuongeza manufaa kwa wakulima.