Watumiaji wakubwa wa maji kutoka Sekta Binafsi na Sekta ya Umma wametakiwa kutimiza jukumu lao la malipo ya huduma wanayoipata ili kazi ya kuimarisha vyanzo vya maji ifanyike kwa ukamilifu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) ametaka malipo ya madai hayo kufanyika akiongoza kamati hiyo kukagua udabuaji na ujenzi wa kingo za mto Lumemo, Kilombero mkoa wa Morogoro.
Mhe. Kiswaga amesema malipo hayo yanasaidia sio tu katika utunzaji na uendelazaji wa vyanzo vya maji bali pia kutoa suluhu zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwamo mafuriko.
Amesema kazi ya udabuaji ni endelevu hivyo inahitaji fedha wakati wote ili maisha ya wananchi yawe salama endapo maji yanazidi katika mkondo wake, akitolea mfano eneo la Ifakara ambapo mavuriko yamekua kero katika shughuli za wananchi za kila siku.
Kazi ya udabuaji na ujenzi wa kingo katika maeneo korofi katika mto Lumemo imegharimu kiasi cha shilingi milioni 294 na kufanikisha eneo lote itagharimu takribani shilingi bilioni 2.2
Pamoja na hilo, Mhe. Kiswaga ameiongoza kamati kukagua mradi wa maji wa miji 28, ambao utekelezaji umefika asilimia 95.
Amesema suala la vifaa na bidhaa za kiufundi zinazoagizwa nje ya nchi zipewe kipaumbele kufika katika eneo la kazi ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma ya maji katika kata sita za Kilombero.
Amesema mradi huo utazalisha kwa siku maji lita za ujazo milioni 20 wakati mahitaji hivi sasa ni lita milioni 10.
Mhe. Kiswaga ameelekeza viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, wawashirikishe wananchi katika kulinda na kuthamini vyanzo vya maji kwa sababu kukamilika kwa mradi huo huduma ya maji itapatikana kwa asilimia 100.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, kwa niaba ya Waziri wa Maji ameainisha kuwa maelekezo yote ya kamati yatafanyiwa kazi ikiwamo kuhakikisha vifaa vya mradi havikwami na kukutana na wadau wanaotegemea huduma ya maji kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo kuona namna bora ya kulipa madeni.

