Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (katikati) akizindua Baraza la 14 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), jijini Dodoma, akishuhudiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Joseph Kuzilwa (kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Hozen Mayaya.
Na Farida Ramadhani na Abdul Iddy, WF – Dodoma.
Serikali ameliagiza Baraza la 14 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kuhakikisha Chuo hicho kinakuwa kitovu cha maarifa, tafiti na utaalamu utakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa Dira 2050.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) katika uzinduzi rasmi wa Baraza hilo.
Mhe. Luswetula alisema Chuo hicho kina nafasi muhimu katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa kupanga na kusimamia maendeleo, hivyo kinapaswa kuhakikisha programu zake za mafunzo, tafiti na ubunifu zinaendana na mahitaji ya uchumi wa sasa na wa baadaye.
Alisema Dira 2050 inatambua elimu na ujuzi kama msingi wa kujenga rasilimali watu yenye maarifa, umahiri na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia hivyo Baraza lihakikishe kuwa Dira hiyo inaakisiwa kikamilifu katika mipango, programu za mafunzo, tafiti na ushirikiano wa Chuo na wadau wake.
“Baraza lina wajibu wa kuongeza msukumo na kuisimamia Menejimenti ili kuongeza uwekezaji katika utafiti na maendeleo (Research & Development), kuimarisha uwezo wa Chuo kufanya tafiti zenye tija na matokeo ya tafiti yanatumika kubuni teknolojia, kuboresha bidhaa na huduma, kuongeza tija na kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi” alisisitiza Mhe. Luswetula
Aidha Mhe. Luswetula, aliliagiza Baraza hilo pia kuhakikisha maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanatekelezwa kwa vitendo na kuingizwa katika mipango, mikakati, bajeti na mifumo ya kupima utendaji wa Chuo.
Alisema maagizo hayo yaliyotolewa kupitia Makamu wa Rais katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026), kilichofanyika Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30, 2026, yanahusu utekelezaji wa Dira ya 2050, kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma, kuwekeza kwa vijana kupitia ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
“Isimamieni Menejimenti kuweka malengo yanayopimika, kutumia rasilimali kwa tija, kuimarisha matumizi ya teknolojia na ubunifu, na kupanua ushirikiano na sekta binafsi pale inapofaa. Vilevile, hakikisheni kuwa uwekezaji katika elimu na ujuzi unaendana na mahitaji halisi ya uchumi na soko la ajira”, aliagiza Mhe. Luswetula
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha nidhamu ya bajeti, kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha, kudhibiti gharama zisizo za lazima, kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana na mapato ya Chuo yanakusanywa na kusimamiwa ipasavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Joseph Kuzilwa aliahidi kuwa baraza hilo litakisimamia Chuo hicho kikamilifu kuhakikisha kinafikia malengo kusudiwa.
Alisema mafanikio yaliyopatikana chuoni ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Baraza, Menejimenti, watumishi na wanafunzi.
Awali akizungumzia mafanikio ya Chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya alisema katika kipindi cha uongozi wa Baraza la 13, Chuo kimepiga hatua katika kuimarisha ubora wa elimu, tafiti na ubunifu.
Alisema Chuo hicho kimeendelea kukuza ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Kituo chake cha Kukuza Biashara na ubunifu, ambapo baadhi ya vijana walionufaika wameanzisha biashara na kuanza kuajiri vijana wengine.
Prof. Mayaya alisema katika kuimarisha uwezo wa taasisi, Chuo kimepanua ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi kupitia mikataba ya makubaliano, ikiwemo kushirikiana na Wizara ya Fedha katika tafiti zinazosaidia kuboresha sera za bajeti na mipango ya Serikali.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) akizungumza wakati akizindua Baraza la 14 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), jijini Dodoma.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Hozen Mayaya akizungumzia mafanikio ya chuo hicho katika uzinduzi wa Baraza la 14 la Uongozi wa hicho, jijini Dodoma.

Meza kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (katikati), Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Joseph Kuzilwa (kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Hozen Mayaya, wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya chuo hicho, baada ya hafla ya kuzindua Baraza la 14 la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha – Dodoma)
