Kuwafundisha watoto matumizi sahihi ya barabara wakiwa katika umri mdogo inatajwa kuwa hatua muhimu inayoweza kusaidia kujenga kizazi chenye nidhamu ya kuzingatia sheria za usalama barabarani na kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.

Hayo yameelezwa na Afisa kutoka kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Dodoma kitengo cha elimu SGT Ester Makali, wakati akizungumza na washiriki wa programu ya VIA – Global Road Safety Education via a New Generation, iliyolenga kuwajengea watoto na vijana uelewa kuhusu matumizi salama ya barabara.

SGT Makali amesema elimu hiyo inapaswa kuanza mapema ili watoto waweze kujenga mazoea sahihi wanapotumia barabara, ikiwemo kujua namna salama ya kuvuka, kutambua alama za barabarani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.

“Kuwajengea watoto uelewa huo tangu wakiwa wadogo kunaweza kuwasaidia kuwa watumiaji wa barabara wanaowajibika wanapokua pamoja na kuifikisha elimu hiyo kwa familia na jamii zinazowazunguka,”amesema

Kwa upande wao, wanafunzi walioshiriki katika programu hiyo wamesema elimu waliyoipata imewapa uwezo wa kutambua vihatarishi vya ajali na kuona umuhimu wa kushiriki katika kutafuta suluhisho, huku wakiahidi kuifikisha elimu hiyo kwa jamii kupitia shule, mitandao ya kijamii na maeneo wanayoishi.

Wanafunzi hao pia wameelekeza umuhimu wa kuimarisha elimu kwa madereva wa bodaboda kuhusu uzingatiaji wa sheria za barabarani, ikiwemo umiliki wa leseni na matumizi sahihi ya barabara.

Kupitia programu hiyo, watoto na vijana wanahamasishwa kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa kutumia maarifa na ubunifu kuelimisha wenzao, familia na jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za barabarani.

Hatua hiyo inaweka msisitizo kuwa mapambano dhidi ya ajali za barabarani yanahitaji ushiriki wa kila mmoja, wakiwemo wanafunzi ambao wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.