Afisa Mawasiliano wa kampuni hiyo, George Naivasha akizungumza na waandishi wa habari jijini ArushaMtaalamu wa ufundi msambazaji wa bidhaa za kampuni hiyo Tanzania ,Dennis Kipsop akizungumza jijiji Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Kampuni ya Stihl East Africa Ltd imetumia maonesho ya Horticultural yanayoendelea jijini Arusha kutangaza teknolojia zake za mashine za kisasa zinazolenga kurahisisha shughuli za kilimo, misitu na usafi wa mazingira.
Afisa Mawasiliano wa kampuni hiyo, George Naivasha, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo unalenga kukutana na wakulima, wadau wa kilimo na kampuni mbalimbali zinazotumia au zinazohitaji kutumia mashine zinazozalishwa na kusambazwa na kampuni hiyo.
Amesema Stihl East Africa Ltd ni kampuni yenye asili ya Ujerumani ambayo imekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka 100, ikiwa na shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya, huku Tanzania ikiwa na wasambazaji wake waliopo Dar es Salaam na Arusha.
Naivasha amesema kampuni hiyo imeamua kushiriki maonesho hayo ili kujitangaza zaidi nchini Tanzania na kuwawezesha wakulima kufahamu namna teknolojia zao zinavyoweza kuboresha shughuli za uzalishaji na kurahisisha kazi za kila siku mashambani.
Ameongeza kuwa mashine wanazozisambaza zina matumizi mbalimbali katika kilimo, ikiwemo kupulizia dawa za mimea pamoja na kukata na kupunguza majani katika maeneo ya mashamba, hatua inayosaidia wakulima kuboresha mazingira ya uzalishaji.
Naivasha amesema kampuni hiyo haijikita katika kuuza mashine pekee, bali pia inatoa huduma za vipuri (spare parts), mafunzo ya matumizi sahihi ya mashine pamoja na namna ya kuzifanyia matengenezo ili kuhakikisha zinadumu na kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha ametoa wito kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo kutembelea banda la Stihl East Africa Ltd ili kujionea teknolojia hizo na kupata maelezo kuhusu matumizi na huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.
Amesisitiza kuwa mashine hizo zinatumia teknolojia ya Kijerumani inayolenga kutoa uimara na ubora, huku upatikanaji wa vipuri na mafunzo ya kiufundi ukiwa sehemu ya huduma wanazowapatia wateja wao.
Kwa upande wake Mtaalamu wa ufundi msambazaji wa bidhaa za kampuni hiyo Tanzania ,Dennis Kipsop amesema kampuni hiyo inatoa mashine mbalimbali zinazotumika katika sekta za kilimo, misitu, utunzaji wa mandhari na usafi, ikiwa na lengo la kuhakikisha wakulima na wadau wengine wanapata vifaa vinavyorahisisha shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kuwa mbali na kusambaza mashine hizo, kampuni pia inatoa huduma za ushauri kwa wateja ili kuwasaidia kuchagua mashine inayokidhi mahitaji yao kulingana na aina ya kazi wanayotaka kufanya.
Dennis amesema huduma nyingine zinazotolewa ni mafunzo ya matumizi ya mashine, kuunganisha vifaa (assembly), pamoja na matengenezo na ukarabati pale mashine zinapopata hitilafu.
Aidha, amesema kampuni hiyo hushirikiana na wakulima kwa kuwapatia elimu na maelekezo kuhusu namna bora ya kutumia mashine mbalimbali ili kuboresha shughuli za kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesisitiza kuwa lengo la Chemalin Engineering Ltd ni kuhakikisha wakulima wanapata teknolojia na vifaa vinavyowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, akibainisha kuwa kilimo ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa nchi.

