Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali inatarajia kutumia takribani shilingi bilioni 204 kukamilisha Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Njia ya Jua Awamu ya Pili wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 100 (MW 100) mkoani Shinyanga, akieleza kuwa mafundi tayari wamewasili katika eneo la mradi kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Mhe. Salome ameeleza hayo leo Novemba 8, 2026, wakati akishiriki ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi wilayani Kishapu.
Amesema mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza uzalishaji wa nishati nchini na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kishapu na maeneo jirani.
Akizungumzia mafanikio ya Awamu ya Kwanza ya mradi huo, Mhe. Salome ameeleza kuwa utekelezaji wake umeleta manufaa mbalimbali kwa jamii, ikiwemo ukarabati wa barabara kupitia programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), upatikanaji wa ajira kwa wananchi, pamoja na ujenzi wa madarasa na zahanati.
Ameongeza kuwa, kutokana na Awamu ya Pili kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme mara mbili ya Awamu ya Kwanza, wananchi wanatarajia kupata manufaa makubwa zaidi yatakayochangia kuboresha huduma za kijamii na kuinua uchumi wao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amewahimiza wanawake na wananchi kwa ujumla kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, mkaa mbadala na umeme, ili kulinda mazingira, kuokoa muda na kupunguza changamoto zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida.
Amesema yeye na madiwani wengine wa viti maalumu mkoani Shinyanga wanaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa nguzo za umeme iliyowasilishwa na wananchi, Mhe. Salome amesema Serikali tayari imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya usambazaji wa nguzo ili kuharakisha kuwaunganishia umeme wananchi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha vitongoji vilivyosalia vinafikiwa na huduma ya umeme ili wananchi wa Kishapu waweze kutumia nishati hiyo katika shughuli za kijamii na kiuchumi, zikiwemo uchakataji wa pamba na bidhaa za mifugo, hatua itakayoongeza thamani ya mazao na kuchochea maendeleo ya wilaya hiyo.

