Mkurugenzi wa Kampuni ya ununuzi na usafirishaji wa zao la parachichi nje ya nchi ya Briaco Limited Avocado ,Mary Christian wakati akizungumza kwenye maonyesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026 linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha .WAKULIMA nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya zao la parachichi kwani mahitaji katika soko la kimataifa yanaendelea kuongezeka kutokana na mwamko wa mataifa mbalimbali kuhusu matumizi ya vyakula vyenye manufaa kwa afya.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi wa Kampuni ya ununuzi na usafirishaji wa zao la parachichi nje ya nchi ya Briaco Limited Avocado ,Mary Christian wakati akizungumza kwenye maonyesho ya jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Bustani, HortiLogistica Africa 2026 linalofanyika katika viwanja vya TGT jijini Arusha.

Mary amesema kampuni hiyo inayojihusisha na usafirishaji wa parachichi nje ya nchi, huku soko lake kubwa ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kupitia Dubai ambayo hutumika kama kituo cha kusambaza bidhaa hizo katika mataifa mengine.

“Ongezeko la mahitaji ya parachichi duniani linatokana pia na kuwa na mafuta yenye manufaa kwa mwili wa binadamu, huku likitumika katika milo mbalimbali ya kila siku.”amesema Mary .

Amesema uzalishaji wa zao hilo nchini unaendelea kuenea katika mikoa mbalimbali, ambapo mbali na Njombe, Iringa na Mbeya, sasa mikoa mingine ikiwemo Katavi imeanza kujikita katika kilimo cha parachichi.

Aidha Mary ameiomba Serikali kuimarisha huduma za usafirishaji na miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayoharibika haraka, akibainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara hulazimika kutumia Bandari ya Mombasa nchini Kenya.

Amesema maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yakipewa kipaumbele kwa mazao freshi yanayohitaji kusafirishwa kwa haraka yanatarajiwa kuongeza matumizi ya bandari hiyo na kuimarisha ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya nje.

“Ushiriki wa kampuni hii katika maonesho haya inalenga kutoa elimu kuhusu fursa za masoko, mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa na kuwaunganisha wakulima, wasafirishaji na wanunuzi kwa ajili ya kukuza biashara ya parachichi.”amesema Mary .

Aidha amewataka wadau mbalimbali kujitokeza katika maonesho hayo ili kujifunza fursa zilizopo, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja itakayoongeza uzalishaji na kukuza biashara ya parachichi nchini.