



Na MWANDISHI WETU (BALTAZAR MASHAKA), UKEREWE
WAUMINI wametakiwa kuendeleza upendo, mshikamano na ushirikiano katika jamii kwa kutenda mema, wakizingatia kuwa maisha ya mwanadamu yana mwisho na kila mmoja anapaswa kujiandaa kwa maisha ya baada ya kifo.
Wito huo umetolewa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kagunguli, Padri Ibrahim Tumaini, wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kifo cha Baltazar Mfungo Buhatwa, iliyofanyika katika Kijiji cha Bulamba, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza.
Ibada hiyo iliyofanyika leo, nyumbani kwa marehemu huyo, ilihudhuriwa na wanafamilia, ndugu wa ukoo wa Wasindi, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho pamoja na waumini wa Kanisa Katoliki, Kigango cha Bulamba.
Katika mahubiri yake, Padri Tumaini alisema kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, baada ya kifo mwanadamu hukabiliwa na hali tatu za maisha ya baadaye, ambazo ni Toharani, Motoni na Mbinguni.
Alisisitiza umuhimu wa kuishi kwa upendo, kushirikiana na wengine na kutenda matendo mema, akieleza kuwa kila mmoja anapaswa kuzingatia mwenendo wake wakati wa uhai ili aweze kupata uzima wa milele.
Katika kuelezea umuhimu wa kutubu na kumtegemea Mungu, Padri Tumaini alitoa mfano wa Yesu Kristo aliyesulubiwa pamoja na wahalifu wawili, mmoja upande wa kushoto na mwingine wa kulia.
Alisema mhalifu aliyekuwa upande wa kushoto alimkejeli Yesu, akimtaka kama kweli alikuwa Mwana wa Mungu ajiokoe mwenyewe na kuwaokoa pia, huku yule aliyekuwa upande wa kulia akimkemea mwenzake kwa kumwambia kuwa wao walistahili adhabu kwa makosa yao, lakini Yesu hakuwa na kosa.
Padri Tumaini alisema mhalifu huyo alimwomba Yesu amkumbuke atakapoingia katika ufalme wake, naye Yesu akamwahidi kuwa siku hiyo angekuwa pamoja naye peponi (kama inavyoelezwa katika Injili ya Mathayo 27:38–44 na Luka 23:39–43). .
Alitumia mfano huo kusisitiza kuwa mwanadamu anapaswa kutambua makosa yake, kutubu na kumtegemea Mungu, huku akihimiza waumini kuishi kwa upendo na kutenda mema katika maisha yao ya kila siku ili wakfa waende mbinguni.
Aidha, aliwahimiza waumini kuwakumbuka marehemu kwa kuwaombea ili Mungu awasamehe makosa yao na kuwapa pumziko la milele.
Kwa upande wake, mtoto mkubwa wa marehemu, Baltazar Mashaka, akizungumza kwa niaba ya familia, alisisitiza umuhimu wa upendo na kuishi kwa amani na jamii, akisema baba yao alikuwa mtu mcha Mungu aliyethamini maadili mema na aliishi kwa wema na jamii.
Alisema marehemu alitumia muda mwingi kuwausia watoto wake kuiga mwenendo na tabia yake, kuishi kwa wema na watu wengine na kuepuka mafarakano katika jamii, hivyo familia itaendelea kumkumbuka kwa mafundisho na maadili aliyowaachia, hasa upendo, kumcha Mungu na kuishi vizuri na watu wengine.
