Amwelekeza Katambi kutoshikilia vitendea kazi kwa makosa ya faini

Ataka maandalizi ya barabara ya Kolandoto–Kishapu–Lalago yaharakishwe

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaruhusu wanunuzi mbalimbali kununua pamba katika msimu unaofuata ili kuongeza ushindani wa bei na kuwanufaisha wakulima.

Amesema hayo leo (Jumapili, Novemba 8, 2026), wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya SHIRECU, wilayani Kishapu, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga.

“Na mimi kama kiongozi wa shughuli za Serikali, nawatangazia kuanzia leo, msimu huu unaofuata hapatakuwa na mnunuzi mmoja. Pataruhusiwa wanunuzi wanunue ili pamba iweze kupanda bei,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema hatua hiyo inajibu malalamiko ya wakulima yaliyowasilishwa pia na Mbunge wa Kishapu, Lucy Thomas Mayenga, kuhusu changamoto za mfumo wa mnunuzi mmoja.

Awali, Mayenga amesema mfumo huo unawanyima wakulima nafasi ya kuchagua wanunuzi na kujadiliana bei, huku baadhi yao wakipata matatizo wanapotafuta masoko katika maeneo mengine.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Paschal Katambi, kuhakikisha wananchi wanaofanya makosa ambayo adhabu yake ni faini wadaiwe faini bila kushikiliwa vitendea kazi vyao.

Amesema kushikilia bodaboda, bajaji na magari kwa muda mrefu kunawazuia wananchi kuzalisha kipato na kuwafanya washindwe kulipa faini wanazodaiwa.

“Kama jambo lao ni faini, viongozi wetu wa Serikali daini faini, mrudisheni kitendea kazi, aendelee na kazi,” amesema.

Amesisitiza kuwa mamlaka zinapaswa kuheshimu mitaji ya wananchi kwa kuwa baadhi ya vitendea kazi hivyo vimenunuliwa kwa mikopo na vinategemewa kuendesha familia.

Kuhusu miundombinu, Dkt. Mwigulu ameitaka Wizara ya Ujenzi kuharakisha uhuishaji wa usanifu wa barabara ya Kolandoto–Kishapu–Lalago ili iingizwe katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Amesema maandalizi hayo yazingatie mahali barabara itakapopita, mahitaji ya madaraja na fidia kwa wananchi watakaoguswa na ujenzi.

Akieleza changamoto hiyo, Mayenga amesema usanifu wa barabara ulifanyika mwaka 2017, lakini wananchi wameendelea kupata usumbufu wa usafiri, uharibifu wa bidhaa na kuchelewa kuwafikisha wagonjwa hospitalini.

Vilevile, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Maji kupanga utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia maeneo yenye ukame na changamoto kubwa ya maji, likiwemo Jimbo la Kishapu.

Kwa upande wa afya, amesisitiza kuwa wagonjwa wa dharura wapatiwe matibabu kwanza bila kucheleweshwa na taratibu za usajili. Pia, amekataza kuwachangisha wagonjwa fedha za mafuta ya ambulansi za Serikali.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesema ataitisha taarifa kuhusu suala la SHIRECU lililowasilishwa na Mbunge wa Kishapu ili Serikali iweze kulifanyia kazi.

Amewapa pia pole wananchi wa kaya takribani 57 zilizoathiriwa na upepo na mvua, akieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeelekeza uongozi wa Mkoa kuratibu hatua za kuwasaidia.