Harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Parokia ya Teule, Mwilamvya mkoani Kigoma, imekusanya takribani Shilingi milioni 137, huku Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Chemba za Biashara za Afrika (PACCI), Bw. Vicent Minja, akichangia Shilingi milioni 10 kusaidia ujenzi wa kanisa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya harambee hiyo, Bw. Minja amesema ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za kijamii ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuchochea maendeleo ya jamii.
Katika mazungumzo hayo, amewahimiza wananchi na waumini kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha zao la mhogo, akieleza kuwa zao hilo lina fursa kubwa za kibiashara kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake katika masoko ya kimataifa, hususan nchini China.
Pamoja na mhogo, amewahimiza wananchi kujikita katika uzalishaji wa mazao mengine yenye fursa za kibiashara, yakiwemo mahindi na asali, kwa kuzingatia mbinu bora za uzalishaji, uchakataji na kuongeza thamani ili kunufaika na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuwahamasisha waumini kujikita katika shughuli za kilimo na ufugaji nyuki kama njia ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Amesema TNCC iko tayari kushirikiana na wakulima na wadau wengine wa sekta binafsi katika kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa fursa za biashara zitakazosaidia kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya jamii.
Bw. Minja amesisitiza kuwa ushiriki katika shughuli za kijamii, ukiambatana na uwekezaji katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya wananchi.

