Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa umeratibu, kwa kushirikiana na Lux Collective Tanganyika na kwa ufadhili wa shirika la ndege la RwandAir, ziara maalumu ya waendeshaji wa utalii kutoka Ufaransa kwenda Tanzania kujionea vivutio na huduma za utalii wa hadhi ya juu.
Kabla ya kuondoka Paris, waendeshaji hao waliagwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, ambaye aliwatakia safari njema na kuwakaribisha kufurahia uzuri wa Tanzania, utajiri wa tamaduni zake na ukarimu wa Watanzania.
Akizungumza wakati wa kuwaaga, Balozi Yakubu alieleza kuwa kuvutia watalii kutoka Ufaransa ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Ubalozi. Alibainisha kuwa idadi ya watalii kutoka Ufaransa wanaotembelea Tanzania kwa sasa imevuka 160,000 kwa mwaka, huku nchi hiyo ikiwa na fursa kubwa ya kupeleka watalii wengi zaidi Tanzania. Alisisitiza kuwa ziara hii ni muhimu kwa Tanzania, kwani itawawezesha waendeshaji hao kujionea vivutio na ubora wa huduma za utalii nchini, na hivyo kuimarisha uwezo wao wa kuitangaza Tanzania na kuwahamasisha Wafaransa wengi zaidi kuitembelea.
Katika ziara hiyo, washiriki watatembelea Zanzibar, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Grumeti. Watapata fursa ya kujionea mchanganyiko wa kipekee wa fukwe, wanyamapori, mandhari na huduma za utalii zinazoiweka Tanzania miongoni mwa maeneo bora ya utalii duniani.
Lux Collective Tanganyika ni mshirika wa muda mrefu wa Tanzania, ambaye ameonesha imani katika sekta ya utalii nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika hoteli ya Marijaan Lux iliyopo Zanzibar. Uwekezaji huo unaakisi dhamira ya kuendeleza utalii wa hadhi ya juu, kuchangia ajira na kukuza utalii endelevu unaonufaisha jamii.
Ubalozi unathamini ushirikiano wa Lux Collective Tanganyika na ufadhili wa RwandAir katika kufanikisha ziara hii, inayounganisha juhudi za diplomasia na sekta binafsi katika kuitangaza Tanzania. Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha mahusiano ya kibiashara katika sekta ya utalii na kuongeza wageni kutoka Ufaransa, ambalo ni mojawapo ya masoko muhimu ya utalii kwa Tanzania.

