Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

7,Novemba 2026

WAFANYAKAZI wa viwandani wametakiwa kuhakikisha wanaelewa masharti yote ya mikataba ya ajira kabla ya kuisaini ili kuepuka migogoro na changamoto zinazoweza kujitokeza katika uhusiano wao na waajiri.

Ushauri huo umetolewa Novemba 6,2026 kupitia Timu ya Wataalamu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Manispaa Kibaha iliyowafikia wafanyakazi wa viwanda mbalimbali vilivyopo Kata ya Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Katika ziara hiyo, wafanyakazi wamepatiwa elimu kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuingia mikataba ya ajira, huku wakipewa nafasi ya kuuliza maswali na kueleza changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa mikataba hiyo na kupatiwa ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa sheria.