NA DENIS MLOWE, IRINGA

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambaye pia ni Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Mohammed Abood, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhishwa na juhudi zinazofanywa na viongozi pamoja na wananchi wa mkoa huo katika kuimarisha chama, kudumisha amani na kusukuma mbele maendeleo.

Abood aliyasema hayo mara baada ya kupokelewa katika Ofisi za CCM Mkoa wa Iringa, ambapo aliwapongeza viongozi wa chama, wanachama na wananchi kwa ushirikiano wanaouonesha katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kupokea miradi inayotekelezwa na Serikali.

Alisema juhudi za wananchi wa Iringa katika kujenga chama, kuimarisha umoja na kushirikiana na Serikali zimetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoufanya mkoa huo kuendelea kuwa mfano katika kudumisha amani na utulivu.

Akitoa salamu za Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema kuwa amefurahishwa na namna wananchi wanavyoshiriki katika maendeleo, huku akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kutekeleza mambo makubwa zaidi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Iringa na Watanzania kwa ujumla.

Abood alisema mafanikio ya maendeleo yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu, hivyo kuwataka viongozi na wananchi kuendelea kulinda misingi hiyo ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa ufanisi.

“Pale ambapo kuna amani na utulivu, ndipo maendeleo makubwa yanapopatikana. Iringa imekuwa sehemu yenye amani na utulivu, na tunataka hali hiyo iendelee kudumu,” alisema.

Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya CCM, Serikali na wananchi umechangia kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwenda vizuri, akiwapongeza wananchi kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alimshukuru Abood kwa kutembelea ofisi za chama hicho na kueleza kuwa mapokezi yake yalionesha hamasa na mshikamano mkubwa miongoni mwa viongozi na wanachama.

Yassin alisema mkoa huo uko tayari kuendelea na shughuli za chama, ikiwemo tathmini ya utekelezaji wa majukumu na mipango ya kisiasa, huku akimkaribisha Abood kuwasalimia wanachama kabla ya kuendelea na kikao.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, James Mgego, alimkaribisha Abood na kumpa nafasi ya kuwasalimia viongozi na wanachama waliohudhuria mapokezi hayo.