Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Nov 6,2026

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imehimiza utunzaji na usimamizi wa sarafu huku ikiwataka wananchi kuacha tabia ya kurushiana ama kuzitupa noti chini, wakati wakitunzana , na badala yake kutumia vifaa maalumu kwa ajili ya kuzihifadhi ili kuzuia uharibifu na kuzifanya zidumu kwa muda mrefu.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha utunzaji wa sarafu ya Tanzania, baada ya kubainika kuwa baadhi ya wananchi hawana utamaduni mzuri wa kutunza fedha, hali inayochangia noti kuchafuka, kuchanika na kuchakaa kabla ya muda wake.

Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa fedha, Ofisa wa Benki Kuu , Kurugenzi ya Sarafu, Shadrack Mapunda alieleza, moja ya changamoto ni baadhi ya wananchi kuonekana kuthamini zaidi dola za Marekani kuliko noti za Shilingi ya Tanzania. 

Alisema noti zinapochakaa na kushindwa kufaa kwa matumizi, BoT huziondoa kwenye mzunguko na kuziharibu kwa mujibu wa taratibu, jambo linalolazimu kuzalisha na kusambaza noti nyingine, hivyo kuongeza gharama ambazo zingeweza kupunguzwa kwa utunzaji madhubuti wa fedha.

Vilevile alisisitiza kuwa uharibifu wa makusudi wa noti ni kosa la jinai, ambapo mtu anayepatikana na hatia ya kuharibu noti anaweza kutozwa faini ya Shilingi 500,000 kwa kila noti au kifungo cha mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria.

Mapunda alisema elimu kuhusu utambuzi wa alama za usalama na utunzaji wa fedha inaendelea kutolewa ili kuwajengea wananchi uelewa kuhusu matumizi sahihi ya noti, kutambua fedha halali na wajibu wao katika kulinda sarafu ya Tanzania. 

Ameongeza kuwa wananchi wenye noti zilizochakaa au kuharibika bila kukusudia wanaweza kuzipeleka benki kwa ajili ya kufanyiwa tathmini na kubadilishwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.