Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetumia mkutano wa wabunge wanawake wa Ukanda wa Maziwa Makuu kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu matumizi sahihi ya takwimu rasmi na umuhimu wake katika kufanya maamuzi na kupanga mipango ya maendeleo.

NBS imeshiriki mkutano huo uliofanyika kwa siku nne, kuanzia Novemba 2 hadi 5, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, ikiwa pia ni miongoni mwa wadhamini wa mkutano huo.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa NBS katika mkutano huo, Noela Masawe, Mtakwimu Mwandamizi kutoka ofisi hiyo, amesema mkutano huo umeipa taasisi hiyo fursa ya kukutana na wadau na watumiaji wa takwimu kutoka nchi mbalimbali.

Amesema kupitia mkutano huo, NBS imepata nafasi ya kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya takwimu rasmi nchini, pamoja na kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu nafasi ya takwimu katika kufanya maamuzi na kupanga mipango ya maendeleo.