Na Mwamvua Mwinyi-

Novemba 6,2026

WADAU wa maendeleo wa Sekta ya Nishati wameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma hiyo, inayotajwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akifungua Kikao Kazi cha Pili cha Mwaka cha Wadau wa Maendeleo wa Sekta ya Nishati kilichofanyika Kisawani, Wilaya ya Mafia, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema nishati ya umeme ni nyenzo muhimu ya maendeleo na kwamba vijiji zaidi ya 12,300 vya Tanzania Bara vimekwishafikishiwa huduma hiyo.

Amesema upatikanaji wa umeme ni muhimu kwa Mkoa wa Pwani kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji, ikiwemo ujenzi wa viwanda katika maeneo ya vijijini, vinavyohitaji nishati ya uhakika ili kuendesha shughuli za uzalishaji.

Nyongo amesema kuridhishwa kwa wadau hao na utekelezaji wa miradi hiyo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano kati yao na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi na kuchochea maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, amesema kikao hicho kinalenga kupitia utekelezaji wa mpango kazi wa miradi ya nishati pamoja na kuwapatia washirika wa maendeleo taarifa kuhusu namna fedha walizochangia zilivyotumika katika kutekeleza miradi hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema vijiji vyote vya Tanzania vimefikishiwa huduma ya umeme, huku Serikali ikiendelea kuangalia namna ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Ameeleza kuwa hadi mwaka 2025, uwiano wa kaya zinazotumia nishati safi ya kupikia ulifikia asilimia 28.6, akibainisha umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo ili kupanua upatikanaji wake kwa wananchi.