Na Mwamvua Mwinyi
Nov 4,2026
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka mkakati wa kuimarisha uandishi wa habari za uchumi na fedha nchini kwa kuwajengea waandishi uwezo wa kuelewa na kuchambua masuala ya kiuchumi na kifedha, ili waweze kufikisha elimu na taarifa sahihi kwa wananchi, wakiwemo wanaoishi vijijini, kuhusu fursa za kiuchumi na kifedha zinazoweza kuwanufaisha.
Kupitia mafunzo hayo, BoT inalenga kuwawezesha wanahabari kuelewa majukumu ya taasisi hiyo, sera za fedha, mifumo ya malipo na maendeleo ya sekta ya fedha, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa habari na kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kiuchumi.
Akifungua semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za fedha na uchumi jijini Dar es Salaam , Novemba 4,2026 Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayesimamia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Mahfoudh alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa wanahabari kuhusu majukumu ya benki hiyo, maendeleo mapya katika sekta ya fedha na masuala ya uchumi yanayoibuka kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Alisema BoT imekuwa ikiandaa semina hizo katika ngazi ya taifa na kanda kwa lengo la kukuza kada ya uandishi wa habari za uchumi na fedha, kuwawezesha waandishi kuandika habari zenye usahihi na kuongeza uwezo wa kuchambua takwimu, ripoti na taarifa zinazotolewa na benki hiyo kila wiki, robo mwaka na mwaka.
Alisema mafunzo hayo tayari yameanza kuleta matokeo chanya, ikiwemo kuongezeka kwa weledi na usahihi wa habari zinazohusu Benki Kuu pamoja na kuimarika kwa ushirikiano kati ya waandishi na wataalamu wa taasisi hiyo katika kupata ufafanuzi kabla ya kuchapisha taarifa.
Mahfoudh alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya uchumi na fedha, hususan wale waishio vijijini ambao wanahitaji kupata taarifa sahihi kuhusu huduma za kifedha na uchumi.
Alisema katika semina hiyo, wataalamu wabobezi wa BoT watawajengea washiriki uelewa kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia kiwango cha riba cha Benki Kuu, dhamana za Serikali na mchango wake katika kuimarisha masoko ya fedha, mifumo ya kulinda watumiaji wa huduma za fedha na masuala ya mikopo.
Mada nyingine zitahusu mfumo wa taifa wa malipo, usimamizi wa sekta ya fedha ili kuhakikisha uthabiti na ustahimilivu wake pamoja na namna ya kubaini na kuandaa habari zinazotokana na takwimu katika ripoti na taarifa za Benki Kuu.
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa BoT, Vicky Msina, alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari ili kuhakikisha taarifa mbalimbali kuhusu shughuli na majukumu ya taasisi hiyo zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.
Alisema waandishi wa habari ni kiungo na daraja kati ya taasisi hiyo na wananchi, kwani wanasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Benki Kuu.
Msina alisema BoT ina mtandao wa waandishi wa habari ambao imekuwa ikishirikiana nao kwa miaka 15 kupitia kanzidata yake, huku ikiendelea kupanua mtandao huo nchi nzima kwa kuwajumuisha waandishi kutoka vyombo vikubwa vya habari, redio za jamii na televisheni ili kuongeza wigo wa kufikisha taarifa kwa wananchi.

