NA DENIS MLOWE, IRINGA

SERIKALI mkoani Iringa imeahidi kuimarisha ushirikiano na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayotekeleza shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikieleza kuwa mchango wa taasisi hizo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.

Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha mashirika hayo kutekeleza miradi na programu zake kwa ufanisi, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo na vyeti vya utambuzi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo ni wanachama wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO).

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika hayo katika kusaidia utekelezaji wa shughuli za maendeleo, hususan katika maeneo ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuzingatia sheria, taratibu na vipaumbele vya Serikali, ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na tija na kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali mkoani Iringa ya kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kujenga jamii yenye ustawi, kupanua huduma za kijamii na kiuchumi na kuharakisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo endelevu