Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema itatekeleza usanifu wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kiluvya kwa Komba hadi Kituo cha Afya na barabara ya Kwa Sumaye hadi Majumba Sita, wilayani Kisarawe, katika mwaka wa fedha 2027/28.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya barabara hizo zenye jumla ya urefu wa kilomita 12.2 ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Akijibu swali la Mbunge wa Kisarawe, Selemani Saidi Jafo, aliyetaka kujua lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Mhe. Profesa Riziki  Shemdoe alisema Serikali imeendelea kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mwaka.

Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga kiasi cha Sh milioni 132 kwa ajili ya matengenezo ya maeneo korofi katika barabara hizo.

“Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara barabara hizi ili ziweze kupitika katika misimu yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2026/27 Serikali imetenga kiasi cha Sh milioni 132 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi katika barabara hizo,” alisema.

Aliongeza kuwa, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiriwa, barabara hizo zitaendelea kufanyiwa matengenezo kwa tabaka la changarawe ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa wananchi.

“Mheshimiwa Spika, aidha, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo kwa tabaka la changarawe, ambapo usanifu wa ujenzi kwa tabaka la lami utatekelezwa katika bajeti ya mwaka 2027/28,” alisema Waziri huyo.

Kauli hiyo inaweka wazi hatua inayofuata ya Serikali katika kuboresha barabara hizo za Kisarawe, huku wananchi wakiendelea kunufaika na matengenezo ya mara kwa mara kabla ya kuanza kwa maandalizi ya ujenzi wa lami.