Na Silivia Amandius BUKOBA, KAGERA.

Wananchi wa Mkoa wa Kagera na maeneo jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma za madaktari bingwa na bobezi zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bukoba, kuanzia Novemba 3 hadi 6, 2026.

Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Samwel Laizer Leo Nov. 3, mwaka huu ambapo ameeleza kuwa huduma hizo zinazotolewa na wataalamu kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ni fursa muhimu kwa wananchi kupata matibabu ya kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Dkt. Laizer amesema uwepo wa wataalamu hao unalenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza gharama zinazoweza kujitokeza wanapofuata matibabu katika hospitali nyingine za rufaa.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bukoba, Dkt. Museleta Nyakiroto, amewahimiza wananchi wenye mahitaji ya huduma hizo kujitokeza hospitalini, akisisitiza kuwa ujio wa wataalamu hao una manufaa zaidi ya matibabu kwa wagonjwa.

Amesema kupitia huduma hiyo, watumishi wa hospitali pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na madaktari bingwa na bobezi, jambo litakalosaidia kuongeza maarifa, ujuzi na kuimarisha utoaji wa huduma za afya.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema unawasaidia kupata huduma za kibingwa kwa urahisi zaidi huku ukiwapunguzia gharama za usafiri na matibabu.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuendeleza utaratibu huo ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa katika Mkoa wa Kagera.