Vifijo, nderemo na shangwe zilisikika mara baada ya Emilian Ngatunga na Witness Mshigeni kuhitimisha sherehe za ndoa yao ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Wawili hawa ilikuwa chaguo lao la kipekee kwa ajili ya kuanza safari mpya ya maisha yao ya ndoa kufanya sherehe yao ya harusi katika eneo hili lenye mandhari ya kuvutia ambapo kuliifanya siku yao kuwa ya pekee zaidi, yenye furaha na kumbukumbu zisizosahaulika ambazo watazithamini maisha yao yote.
Wakielezea furaha yao, maharusi hao wameonesha kufurahishwa na uamuzi wao wa kuchagua Ngorongoro kuwa sehemu ya kufungia ndoa yao, wakieleza kuwa walipata uzoefu wa kipekee na usioweza kusahaulika.
“Kiukweli Ngorongoro ni sehemu ya pekee kuhitimisha harusi, mapenzi yetu yamekuwa moto moto kwa kufika hapa ni raha juu ya raha, mahaba juu ya mahaba”, walisema wapendao hao.
Ngorongoro inajulikana sana kutokana na historia yake hasa chimbuko la binadamu wa kale na wengine husema kwamba kutokana na historia yake inawezekana tunda la mti wa kati lililiwa katika eneo hilo.

