
TANZANIA inatarajiwa kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo cha hotikacha barani Afrika kupitia jukwaa la kimataifa la HortiLogistica Africa 2026, litakalowakutanisha wakulima, wawekezaji, wafanyabiashara, wanunuzi wa kimataifa, wasafirishaji na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga, matunda na maua kutoka ndani na nje ya nchi.
Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 8 hadi 10 mwaka 2026 katika viwanja vya TGT, mkoani Arusha, likiwa na lengo la kuunganisha wazalishaji wa mazao ya hotikacha na masoko ya ndani na kimataifa, pamoja na kuweka mazingira bora ya kuvutia mitaji na teknolojia mpya katika sekta hiyo.
HortiLogistica Africa 2026, inayoandaliwa na Asasi Kilele ya Sekta Binafsi inayojishughulisha na kuendeleza na kukuza sekta ya hotikacha nchini (TAHA), kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, inatarajiwa kukutanisha wakulima, wasafirishaji, wanunuzi, teknolojia, vionhozi, wafanyabiashara na wataalamu kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.
Umuhimu wa jukwaa hilo hauishii katika maonesho pekee, bali linatoa fursa ya kujenga mahusiano ya kibiashara kati ya wakulima na wanunuzi wakubwa wa kimataifa, kupata mikataba ya kuuza mazao nje ya nchi, kuvutia wawekezaji na kubadilishana teknolojia zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
Aidha, jukwaa hilo linatarajiwa kufungua fursa katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa hotikacha, yakiwemo uzalishaji wa kisasa, upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, vifaa vya kilimo, teknolojia za umwagiliaji, uhifadhi wa mazao, ufungashaji, usafirishaji na huduma za ugavi wa kimataifa.
Katika eneo la biashara ya kimataifa, uwepo wa wanunuzi, wasafirishaji na wawekezaji utatoa nafasi kwa wakulima na kampuni za ndani kupata taarifa za mahitaji ya masoko ya nje, viwango vya ubora vinavyohitajika na namna ya kukidhi masharti ya usafirishaji wa mazao kwenda kwenye masoko mbalimbali duniani.
Pamoja na hayo, matumizi ya teknolojia za kisasa za uhifadhi na usafirishaji wa mazao katika mifumo ya cold chain yanatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya majadiliano, hatua inayoweza kusaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Kwa upande mwingine, jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa vijana na wajasiriamali kuingia katika biashara zinazohusiana na hotikacha, ikiwemo huduma za usafirishaji, usindikaji, ufungashaji, uuzaji wa pembejeo, teknolojia za kilimo na huduma za kifedha.
Aidha, Serikali imekuwa ikitambua sekta ya hotikacha kama eneo lenye uwezo wa kuchochea uwekezaji, kuongeza mapato ya wakulima, kukuza biashara ya nje na kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania.
Kupitia HortiLogistica Africa 2026, Tanzania inalenga kutumia nafasi yake ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki na fursa za miundombinu ya usafiri na masoko ili kujenga mazingira yatakayoiwezesha nchi kuwa kitovu cha biashara na usambazaji wa mazao ya hotikacha barani Afrika.
Kaulimbiu ya jukwaa hilo ni “Bridging Markets, Cultivating Prosperity”, ikimaanisha kuunganisha masoko na kukuza ustawi kupitia kilimo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuendeleza sekta ya hotikacha.
Hivyo, HortiLogistica Africa 2026 inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha uzalishaji na masoko, ambapo mafanikio yake yatapimwa pia kwa uwezo wa kuzalisha mikataba ya biashara, uwekezaji mpya, teknolojia na fursa endelevu kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
