Na. Sophia Kingimali, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Festo Dugange, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mipango ya maendeleo ya majiji nchini ili kukabiliana na ongezeko la watu, kuboresha makazi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii na kiuchumi.
Amesema ongezeko la watu mijini linahitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi, miundombinu ya usafiri na makazi bora ili kuzuia kuongezeka kwa makazi yasiyopangwa na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Miji Duniani yaliyofanyika Oktoba 31, 2026 Jijini Dar es salaam, Dugange amesema Tanzania ina majiji sita ambayo Serikali imeendelea kuyaboresha kupitia ujenzi wa barabara, masoko, vituo vya mabasi na miundombinu mingine muhimu.
Amesema pamoja na miradi ya miundombinu, Serikali imeendelea kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi na kurasimisha makazi yaliyokuwa yamejengwa bila kufuata utaratibu, hatua inayolenga kuyafanya majiji kuwa maeneo salama na yenye ubora wa maisha kwa wananchi.
Dugange amesema watendaji wa Serikali wanapaswa kuhakikisha upangaji wa ardhi unazingatia utaalamu ili kutenganisha maeneo ya viwanda, makazi, shughuli za biashara na maeneo ya wazi yatakayotumika kwa upandaji miti na maua.
Amesema Serikali pia imekubaliana kuimarisha ushirikiano na Wizara ya Ardhi, UN-Habitat na wadau wengine katika kuboresha maeneo ya makazi yaliyopangwa zamani bila kuzingatia mahitaji ya sasa ya mijini.
Ameongeza kuwa ongezeko la watu linahitaji majiji kujiandaa mapema, akitolea mfano Jiji la Dar es Salaam ambalo kwa mujibu wa makadirio ya Serikali linatarajiwa kuwa na wakazi wengi zaidi ifikapo mwaka 2030, hivyo kuhitaji miundombinu na huduma zitakazokidhi mahitaji hayo.
Amesema hatua nyingine inayopaswa kupewa kipaumbele ni kuboresha mifumo ya usafiri na kuanza kuhamia kwenye matumizi ya vyombo vya moto vinavyotumia nishati ya umeme au gesi ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Grace Bubaly, amesema maendeleo ya miji yanapaswa kulenga ustawi wa wananchi badala ya kupimwa kwa wingi wa majengo marefu na mandhari ya kuvutia pekee.
Amesema ongezeko la watu katika Jiji la Dar es Salaam linahitaji mipango endelevu ya matumizi ya ardhi, makazi bora na uhuishaji wa maeneo ya mijini ili kuhakikisha maendeleo yanazalisha thamani ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Bubaly ametaja maeneo ya Ubungo na Mbezi kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kuonesha umuhimu wa mipango bora ya maendeleo ya mijini katika kuongeza thamani ya maeneo na kuboresha maisha ya wakazi.
Naye Meya wa Manispaa ya Ubungo Lawrence Mlaki amesema halmashauri hiyo imeanza kushirikiana na Wizara ya Ardhi katika kupanga upya maeneo ya Sinza ili kuboresha matumizi ya ardhi, akieleza kuwa mpango huo tayari umepitia vikao vya wataalamu na kuwasilishwa kwenye Baraza la Madiwani kwa ajili ya kuidhinishwa.
Mlaki amesema Manispaa ya Ubungo pia imeendelea kutekeleza kampeni ya usafi inayojulikana kama Kausapeu, inayolenga kuhamasisha wananchi kukataa uchafu na kusafisha maeneo yao, huku mitaa ikishindanishwa kwa viwango vya usafi ili kuhamasisha uwajibikaji.
Ameongeza kuwa halmashauri za Dar es Salaam zina mpango wa kutenga asilimia tano ya mapato ya ndani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa masoko, vituo vya mabasi na miundombinu mingine, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi na wananchi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya miji

